RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Mashirika na Taasisi za Umma kuhakikisha yanawajibika ipasavyo katika kulinda na kuendeleza uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika hayo, na kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo ya kiuchumi.
Kwa Mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imeeleza kuwa Rais Dkt. Samia ametoa
wito huo leo katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi na
Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amesema kuwa mageuzi
makubwa yanayotekelezwa na Serikali kwenye usimamizi na uendeshaji wa Mashirika
ya Umma yameanza kuonesha mafanikio, ikiwemo Mashirika 11 kati ya 13 yaliyokuwa
na mtaji hasi kuhamia kwenye kundi lenye mtaji chanya, na Mashirika mengine
nane katika hayo yaliyokuwa yanapata hasara sasa yameanza kupata faida.
Katika kuzidi kuongeza mchango wa Mashirika kwenye uchumi,
Rais Dkt. Samia amemuagiza Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu kuendelea
kuwajengea uwezo watendaji na kuhakikisha mashirika yanaongeza ubunifu na
kuimarisha matumizi ya TEHAMA.
Vilevile,
amemtaka Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya kuangalia namna ya kuongeza
ushiriki wa wananchi katika umiliki wa mashirika kupitia soko la hisa.
Rais Dkt. Samia pia amesisitiza umuhimu wa kutambua
Mashirika na Taasisi ambazo hazitoi mchango wa fedha moja kwa moja kwa
Serikali, bali huchangia kupitia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Serikali imepokea gawio la jumla ya Shilingi Trilioni 1.028
kutoka katika Mashirika na Taasisi za Umma ikiwa ni ongezeko la asilimia 34
ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 767 zilizotolewa mwaka jana.
Aidha, idadi ya Mashirika na Taasisi zilizochangia imeongeza kufikia 213, huku kampuni zenye hisa chache za Serikali zikiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa, zikiwemo Twiga Minerals (Shilingi Bilioni 93.6), Airtel Tanzania (Shilingi Bilioni 73.9) na NMB Bank (Shilingi Bilioni 68.1).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...