RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko, Serikali inaendelea kufanya marekebisho ya sera kwa lengo la kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi wa Taifa.
Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali ni kuhakikisha sera mpya zinatoa msukumo wa kuitambulisha Tanzania kupitia bidhaa na huduma zake, na hivyo kuongeza mapato ya Taifa.
Mwinyi alitoa agizo hilo jana katika ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam alisema wizara zinatakiwa kuhakikisha kuwa elimu ya alama za utambulisho wa bidhaa (branding) inawafikia Watanzania wengi, ikiwa ni chachu ya kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kuhamasisha uzalendo wa kiuchumi.
Alisema ni vema wananchi wapende kutumia bidhaa za ndani, kwani ni njia bora ya kukuza uchumi wa kitaifa na kujenga kujivunia bidhaa zetu wenyewe.
"Hatua za kimkakati zinazotekelezwa zinaenda sambamba na kukuza ubunifu, kushirikiana na sekta binafsi, na kuanzisha madirisha ya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, yote haya yakiwa ni katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji,"alisema
Rais Dkt.Mwinyi alitoa pongezi kwa kuandaliwa kwa mpango kabambe wa uendelezaji wa biashara na kubainisha kuwa uwanja wa kisasa wa biashara unaotarajiwa kujengwa utazingatia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP),na jitihada zikifanywa kuondoa urasimu unaokwamisha maendeleo.
Kw upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, alisema Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu yameendeshwa kwa njia ya kidijitali kutokana na mifumo ya kisasa iliyowekwa.
Latifa alisema hatua hiyo ni sehemu ya mabadiliko kuelekea maonesho ya miaka 50 (Golden Jubilee) mwaka ujao, ambapo TanTrade imejipanga kuyafanya kuwa ya kisasa zaidi na yenye viwango vya kimataifa.
Latifa alisema kuwa pamoja na uendeshaji wa kidijitali, mipango iliyopo sasa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya eneo la maonesho ili kulifanya kuwa la kuvutia zaidi kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mkoa wake unayachukulia Maonesho ya Kila Mwaka ya Kimataifa ya Dar es Salaam kama kielelezo cha mkoa huo kimataifa, na hivyo wataendelea kuyaenzi na kuyaboresha.
Alisema Serikali ya mkoa wake itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade) kuboresha miundombinu ya viwanja vya Sabasaba ili iendane na hadhi ya maonesho hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...