Songea_Ruvuma.

Lamory Arena Sports Bar iliyopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma leo Julai 3 2025, imezinduliwa rasmi  baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa uliodumu kwa miezi mitatu, ukilenga kuboresha huduma kwa wateja na wageni mbalimbali wanaotembelea eneo hilo maarufu kwa burudani na chakula.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile, ambaye alikuwa mgeni rasmi, ameipongeza familia ya mmiliki wa Lamory kwa hatua waliyochukua ya kuboresha miundombinu na mazingira ya eneo hilo.

Amesema ukarabati huo unaonesha dhamira ya dhati ya mmiliki huyo katika kusaidia juhudi za serikali kukuza uchumi wa mji wa Songea.

DC Ndile amesisitiza kuwa serikali ya wilaya ya Songea itaendelea kushirikiana na wamiliki wa maeneo ya biashara kama Lamory, hasa kwa kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa, kwa kuwa maeneo hayo yanahudumia watu wengi na yana mchango mkubwa katika ajira na pato la wilaya.

“Serikali yoyote makini duniani lazima iheshimu biashara za watu, kufungia biashara kiholela ni sawa na kuua ajira na kurudisha nyuma mapato ya wananchi tunapaswa kushirikiana na wafanyabiashara,,” alisema DC Ndile.

Amewaasa Maafisa biashara kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na busara, huku wakitambua kuwa biashara nyingi ni tegemeo kwa familia nyingi, aidha amezitaka taasisi za kifedha kuwa na mtazamo chanya kwa wafanyabiashara kwa kutowahukumu wote kwa makosa ya wachache waliotangulia kushindwa kurejesha mikopo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya hafla hiyo, Yusuf Mwikoki, amesema ukarabati wa Lamory ulilenga kuongeza ubora wa huduma na kuvutia wageni wengi zaidi wanaoingia na kutoka mjini Songea, amesema eneo hilo limebaki kuwa tulivu na salama kwa watu wa aina zote.

“Hatukuwahi kuwa na changamoto yoyote hapa. Tunapokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali na wote wanafurahia huduma, ndiyo maana tuliona umuhimu wa kumwalika mgeni rasmi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kushuhudia maendeleo haya,” alisema Mwikoki.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba, naye ametoa rai kwa wamiliki wengine wa biashara kuiga mfano wa Lamory kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara zao ili kuifanya Songea kuwa mji wa kuvutia zaidi kwa wawekezaji na watalii.

Naye mmiliki wa Lamory Sports Arena, Christopher Limo, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuhudhuria uzinduzi huo na kuahidi kuwa wataendelea kuboresha huduma, kulinda usalama wa wateja na kushirikiana na serikali katika kuendeleza eneo hilo kiuchumi.

Ukarabati wa Lamory Arena si tu umetangaza sura mpya ya eneo hilo, bali pia umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi wilayani Songea, ni  mfano mzuri wa namna ambavyo uwekezaji katika biashara unaweza kuchochea maendeleo, kutoa ajira, na kuongeza mapato ya ndani.

Serikali, taasisi za kifedha, na wafanyabiashara wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuijenga Songea kuwa kitovu cha biashara, burudani, na utalii wa ndani



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...