Na MWANDISHI WETU,


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bi. Mwamini Malemi, amepongeza huduma zinazotolewa kwa wanachama na wananchi wanaotembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo, Bi. Malemi alisema ameridhishwa na namna huduma zinavyotolewa kwa weledi, ufanisi na kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali.

“Nimejionea huduma bora zinazotolewa kwa wanachama na wananchi. Hili linaonyesha kuwa Mfuko umejipanga kikamilifu katika kuwahudumia Watanzania kwa ubora,” alisema Bi. Malemi.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi, hususan wale waliojiajiri, kujiunga na NSSF ili kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye na kunufaika na mafao mbalimbali ikiwemo mafao ya matibabu, mafao ya uzeeni, uzazi, na mengineyo yanayotolewa na Mfuko.

Katika ziara hiyo, Bi. Malemi pia alitembelea mabanda ya kampuni tanzu za NSSF zikiwemo Mkulazi inayojishughulisha na uzalishaji wa sukari, na kampuni ya Sisalana inayozalisha bidhaa za katani. Alisema kampuni hizo ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati wa Mfuko katika kuchochea uchumi wa taifa na kuhakikisha ustawi wa wanachama kupitia ongezeko la thamani ya mafao yao.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Bw. Abdul Zuberi, alisifu juhudi za Mfuko katika kutoa huduma kwa haraka, kwa ufanisi na kwa kutumia teknolojia, hali inayosaidia upatikanaji wa huduma karibu na wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, pia alitembelea banda la Mfuko na kushuhudia namna wanachama na wananchi wanavyohudumiwa.

Alipongeza watendaji wa NSSF kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kusajili wanachama wapya hasa kutoka sekta binafsi na wananchi waliojiajiri, pamoja na kuwahamasisha kutumia mifumo ya kidijitali kama NSSF Portal na NSSF App.

Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanaendelea kuvutia wananchi wengi, huku banda la NSSF likiendelea kutoa huduma, elimu na usajili kwa wananchi waliojiajiri.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...