Na Diana Deus,Missenyi

Wafugaji wa Mkoa wa Kagera wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali za kufikisha mifugo katika vituo vya kutolea chanjo na utambuzi wa mifugo ili kufikia adhima ya serikali ya kudhibiti magonjwa na kupanua wigo wa masoko ya kimataifa.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamis Mahiga, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa wakati wa utekelezaji wa kampeni kimkoa katika wilaya ya Missenyi, amesema ni muhimu wafugaji wakafuata ratiba kama itakavyoainishwa kwa ajili ya mifugo yao kuchanjwa na kutambuliwa.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeridhia kugharamia mpango wa miaka mitano unaoanza 2025 hadi 2029 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 216, kwa ajili ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kote nchini, hivyo ni muhimu wafugaji wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanashiriki vyema kwa kuwa zoezi hilo siyo la hiari bali ni lazima.

Alitoa wito kwa viongozi wenzake kusimamia vyema zoezi la utoaji chanjo na utambuzi ili adhima ya serikali iweze kufikiwa ikiwemo kuhamasisha wafugaji na kutoa elimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael, akimwakilisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti, amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuuza nyama nje ya nchi hususan nchi za Mashariki ya Kati.

Alisema kuwa hadi sasa kuna takriban tani 14,000 ambazo zinaenda kwenye masoko hayo lakini bado kuna masoko kwenye mataifa mengine ikiwemo China na Bara la Ulaya ambayo yanahitaji kuuziwa nyama kutoka Tanzania.

Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inapita maeneo mbalimbali nchini, kuhamasisha Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliizindua Juni 16 mwaka huu mkoani Simiyu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Kagera, Haji Abdul Majid Kayondo, alisema zoezi la chanjo wamekuwa wakilihitaji kwa muda mrefu na kwamba wamelipokea kwa mikono miwili na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema kuwa wenyewe kama chama wataweka hamasa kubwa kwa wafugaji hususan Wilaya ya Missenyi ambayo ni mojawapo ya wilaya yenye mifugo mingi mkoani humo.

Alitoa wito kwa wafugaji kushiriki vyema katika zoezi hilo na kutoficha mifugo ili kufikia adhma ya serikali katika kuwa na mifugo bora na yenye tija.

Serikali imetoa ruzuku kwa chanjo za mifugo katika kampeni hii ambapo kuku wanachanjwa bure, ng’ombe mmoja Shilingi 500 wakati mbuzi na kondoo Shilingi 300 kwa kila mmoja.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...