Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Prof. Fortunata Makene, amesema kuna haja ya nchi za Global South (nchi za Kusini) kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kujitegemea kiuchumi na kupata nafasi kubwa katika utawala wa kimataifa.
Ameyasema hayo leo kwenye mdahalo wa wataalam uliofanyika katika ukumbi wa ESRF, uliolenga "kubadilishana maarifa" juu ya nafasi ya Global South duniani.
"Tulianza ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China mwaka 2017, lakini mwaka jana tulisaini mkataba wa uhusiano ili kuendelea kufanya majadiliano yanayohusisha nchi za Global South," alisema Prof. Makene na kuongeza:"Tunaona ushirikiano unahitajika kwa sababu mifumo yetu ya maendeleo ni tofauti kidogo. Ni muhimu tujadili namna gani nchi hizi zinaweza kushirikiana."
Prof. Makene alibainisha kuwa mdahalo huu umekuja wakati muafaka kutokana na mabadiliko makubwa ya kimataifa. Alitolea mfano wa hatua za Marekani na Uingereza za kupunguza misaada kwa nchi nyingi, jambo lililosababisha sintofahamu na mahangaiko.
"Kama Watanzania na kama Global South, tuna wenzetu wa Kusini wamepitia changamoto za maendeleo lakini wamefika mbali," alisema. "Kuna China, Malaysia, Singapore, na Korea Kusini. Tulijinyakua uhuru pamoja nao lakini wako mbali sana. Tunakosea wapi?"
Aliongeza kuwa tatizo linaweza kuwa linatokana na kujikita zaidi kwenye mifumo ya maendeleo ya nchi za Magharibi au Kaskazini, ambayo inaweza isiendane na mazingira halisi ya Watanzania.
Mmoja wa wataalamu katika mdahalo huo alipendekeza kuangalia namna ya kuweka mfumo wa maendeleo unaomlenga Mtanzania bila kumwondoa sana kutoka kwenye mazingira yake halisi.
Prof. Makene alishangazwa na hali ya nchi za Global South kuhangaika misaada inapokatwa, licha ya kuwa na rasilimali nyingi za kutosha. Alisema Tanzania ina ardhi yenye rutuba na madini mengi, na inaweza kulisha bara zima la Afrika.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na China, ambapo wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha China wamekuwa Morogoro kwa miaka kumi wakifanya kazi ili kuleta mbinu mbalimbali za kilimo ambazo ziliwasaidia China kufanikiwa.
"Tumeamua kushare knowledge (kubadilishana maarifa) na wataalam wetu ili tuweze kujifunza kutoka kwao, na wao wajifunze kutoka kwetu," alisema Prof. Makene. "Kushirikiana ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo endelevu na kujitegemea kiuchumi."
Katika madahalo huo Wanazuoni wa Kitanzania na Kichina wamesisitiza umuhimu wa nchi za Kusini (Global South) kuondokana na utegemezi wa misaada na badala yake kutumia maarifa na rasilimali zao kujiletea maendeleo.
Wamesema hayo katika mdahalo huo wa tatu wa wataalamu wa China na Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa ESRF, jijini Dar es Salaam.
Mdahalo huo, ulioshirikisha wanazuoni kutoka ESRF, Chuo Kikuu cha Kilimo cha China (CAU), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ulijikita katika jukumu la Global South katika utawala wa kimataifa.
Profesa Andrea Kifasi na Profesa Samuel Wangwe walihimiza mataifa kutafuta vyanzo mbadala vya ufadhili wa maendeleo, huku Prof. Wangwe akirejelea falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kujitegemea. Dk. Richard Mbunda alisisitiza umuhimu wa "utawala wa chakula" (food sovereignty) kwa kuwasaidia wakulima wadogo na kupunguza utegemezi wa nje.
Profesa Zhang Lei alisisitiza kuwa Global South ina rasilimali nyingi za kutosha kujenga mifumo yake ya maendeleo na kuhamasisha wananchi wake. Mkutano huo pia ulionesha mafanikio ya ushirikiano kati ya Tanzania na China, ukitoa mfano wa mradi wa kilimo wa "Small Technologies, Big Harvests." unaoendeshwa Morogoro.
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...