Benki ya NMB imeendelea kuimarisha uhusiano na wateja wake visiwani Zanzibar kupitia mikutano ya ana kwa ana na wateja wakubwa, sambamba na kutoa elimu kuhusu masuluhisho mbalimbali inayoyatoa kwa wafanyabiashara.
Ujumbe wa benki hiyo, ukiongozwa na Meneja Biashara wa NMB Zanzibar, Bi. Naima Said Shaame, akiwa ameambatana na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara, Dickson Richard, pamoja na viongozi wengine wa benki, umekutana na wateja wakubwa katika ziara maalum ya kikazi.
Ziara hiyo inalenga kuendeleza ukaribu na kujenga uaminifu kati ya NMB na wateja wake, huku ikilenga kuhakikisha huduma na bidhaa zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya wateja.
Kwa miaka mitatu mfululizo, Benki ya NMB imetambuliwa kama Benki Salama Zaidi Tanzania (Safest Bank in Tanzania) na jarida la Global Banking & Finance Magazine, kuthibitisha ubora wake na kutambulika kimataifa katika nyanja mbalimbali za huduma za kifedha.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Shaame aliwashukuru wateja wote waliohudhuria na kuwasihi waendelee kuwa mabalozi wa Benki ya NMB kwa kuwaleta wateja wapya.
Pia aliwaomba kuhakikisha kuwa mauzo na malipo yote ya biashara zao yanapitishwa kupitia akaunti zao za NMB ili kuongeza fursa ya kupata mikopo mikubwa zaidi kutoka benki yao.
Bi. Shaame aliongeza kuwa ubunifu unabaki kuwa nguzo kuu ya NMB, na benki itaendelea kuibua masuluhisho bora yatakayoongeza tija kwa wateja na kuchochea ukuaji wa biashara zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...