NA WILLIUM PAUL, SAME. 

MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameingilia kati mgogoro wa ardhi baina ya Wakulima na Wafugaji katika kijiji cha Ruvu marwa wilayani Same na kutoa siku 14 kwa Afisa ardhi mkoa na wilaya kwa kushirikia na pande zote mbili kupata suluhu ya matumizi bora ya ardhi hiyo. 

Babu alitoa kauli hiyo jana alipofika kijijini hapo kuzungumza na wananchi hao ambapo pia aliagiza shughuli zote ambazo zilikuwa zikiendelea katika eneo lenye ukubwa wa hekari 2787 kusimama mpaka pale suluhu ya eneo hilo ambalo linagombewa kupatikana. 

"Katika hili eneo la heka 2787, Wafugaji wasiliguse na Wakulima pia katika eneo ambalo mmegawana gawana nalo lisimame katika kipindi cha siku 14, Mkuu wa wilaya, Mkurugenzi wa halmashauri ya Same, Afisa Ardhi, Watu wa kilimo na pia chagueni timu kutoka kwa Wakulima na Wafugaji ili tuweze kupata hatima ya hili eneo ili kumaliza huu mgogoro" Alisema Babu. 

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, pia atatuma wataalam kutoka ofisini kwake kutembelea maeneo ambayo Wakulima wanalima ambayo yamekuwa yakiingiwa na mafuriko kila mwaka ili serikali iweze kuleta vifaa kuhakikisha maji hayaingii katika mashamba ya Wakulima. 

Alisema kuwa, hapo awali Mkuu wa wilaya aligawa hekari 260 kwa wakulima 600 ambao ndio mashamba yao yaliingiliwa na mafuriko lakini zoezi hilo halikufanyika kama lilivyotolewa maelekezo na Mkuu huyo wa wilaya ambapo ziligawanywa hekari zaidi ya 260.

Katika hatua nyingine alimtaka Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambaye amekuwa akitupiwa lawama nyingi za kuegemea kwa Wafugaji katika kufanya maamuzi ya mgogoro huo na kumtaka kuhakikisha anasimama katikati bila kuegemea upande wowote kwani jamii yote ndio ilimchagua kuwaongoza.

Serikali inataka Wakulima na Wafugaji katika kijiji hicho kurudi na kuwa kitu kimoja na kuwataka kuweka amani na utulivu mbele kwani wote ni Watanzania wanapaswa kuishi kwa umoja huku pia akiagiza vyombo vya usalama kuwachukulia hatua wananchi wenye chokochoko za mgogoro huo. 

"Nawaombeni ninyi wananchi wa Ruvu marwa rudisheni mahusiano muwe kitu kimoja mtaishi hivi mpaka lini tujengeni amani hatutaki kuleta polisi huku kila wakati na ninyi ni Watanzania kuhusu swala la Mwenyekiti niachie mimi na chama cha Mapinduzi tutajua nini cha kufanya" Alisema Babu. 

Akisoma risala ya Wakulima kwa Mkuu huyo wa mkoa, Penueli Mkomwa alisema kuwa eneo la bonde la Ruvu wamekuwa na kadhia ya kukumbwa na mafuriko mara kwa mara na kupata hasara kubwa. 

Alisema kuwa, katika kijiji chao lipo eneo la wazi ambalo linaweza kuwa suluhisho kwa Wakulima kulima kwani halifikiwi na mafuriko japo kuwa eneo hilo linazuio la pori tengefu. 

Aliongeza kuwa, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alifika katika kijiji hicho na kuagiza eneo hilo ligawiwe kwa Wakulima waweze kulima kwa muda mpaka pale maji yatakapokauka katika mashamba ya kulima waweze kurudi katika mashamba yao. 

Alisema Wafugaji wamekuwa mstari wa mbele ya kupiga eneo hilo kugawiwa kwa Wakulima hali ambayo imechangia kuwepo kwa mgogoro huo wa Wakulima na Wafugaji. 

Naye Mwenyekiti wa Wafugaji kijiji cha Ruvu marwa, Isaya Lazaro alisema kuwa, eneo hilo la hekari 2787 walishagawiwa kihalali na Serikali kama eneo la Wafugaji kwa ajili ya malisho ya mifugo kwa mujibu wa sheria. 

Lazaro alisema katika hali ya kushangaza walishangaa kuona eneo hilo linachukuliwa bila makubaliano na kuanza kugaiwa kwa Wakulima kama mashamba hali ambayo ndio chanzo cha kuibuka kwa mgogoro huo wa Wakulima na Wafugaji. 







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...