
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa, imekutana na wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa TRA, mawakala wa Forodha na wafanyabiashara mkoani Songwe na kuwapa elimu juu ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mkutano huo uliofanyika Agosti 28,2025 katika mpaka wa Tunduma, wilayani Momba, uliendeshwa na Maofisa Wakuu wa Forodha, Allan Maduhu na Hassan Minga.
Maduhu alisema semina hiyo inalenga kuwajengea uelewa wa pamoja wadau wote wa forodha na biashara ili utekelezaji wa sheria hizo mpya uwe wa ufanisi.
“Leo tumekutana na wadau mbalimbali wakiwemo waagizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi, mawakala wa Forodha na watendaji wa TRA hapa mpakani Tunduma. Tumejadili marekebisho yaliyofanywa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2025, ambayo yamepunguza kodi katika baadhi ya bidhaa ili kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi zaidi,” amesema Maduhu.
Amebainisha kuwa miongoni mwa marekebisho hayo, serikali imepunguza kodi katika bidhaa ya vitenge vinavyoingizwa nchini, hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wananchi na kuongeza ushindani wa biashara.
Sambamba na hayo, serikali pia imetoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gesi ya kupikia pamoja na mitungi na matanki yake, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza gharama kwa watumiaji.
Kwa upande wake, Nsajigwa Mwambegele Meneja Msaidizi wa Forodha, amesema serikali imesikiliza kilio cha wananchi na kupunguza kodi kutoka asilimia 50 hadi asilimia 35, akibainisha kuwa hatua hiyo itapunguza magendo.
“Kupunguza kodi kutawafanya wananchi waachane na njia zisizo rasmi za kuingiza bidhaa kwa kuwa viwango vya sasa ni himilivu,” amesema.
Naye Djuma, mfanyabiashara wa vitenge kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amesema afuwa hiyo ya kodi italeta nafuu kubwa kwa wafanyabiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kupunguza kodi ni jambo la heri kwa sababu kutanyanyua biashara zetu na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa sokoni,” amesema Djuma.
Kwa ujumla, TRA imewataka wafanyabiashara wote kutumia njia rasmi za kuingiza bidhaa nchini ili kunufaika na afuwa za kikodi na kuepuka kukinzana na sheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...