Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Tanzania leo imeadhimisha kwa mara ya kwanza kitaifa Siku ya Kimataifa ya Mikoko Duniani, kwa kupanda jumla ya miti 5,000 ya mikoko katika eneo la Kilongawima, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam – ikiwa ni hatua muhimu katika kulinda mifumo ikolojia ya ardhi oevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Siku ya Mikoko Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Julai kote duniani, ambapo nchi mbalimbali hupewa fursa ya kuandaa matukio ya maadhimisho kulingana na hali ya hewa, mazingira, na ratiba zao za ndani.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, aliwataka viongozi wa mitaa, kata, wananchi na wadau wa mazingira kushirikiana katika kulinda mikoko kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

“Tukitunza mikoko tunahifadhi mazingira yetu, tunalinda maisha, na tunajenga uchumi wa jamii. Linda ardhi oevu kwa ustawi wa maisha ya sasa na yajayo,” alisisitiza.

Maadhimisho hayo yaliyopewa kaulimbiu: “Linda Ardhi Oevu kwa Ustawi wa Maisha ya Sasa na Yajayo”, yamehudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo TFS, IUCN, WWF, Wetlands International, Earth Lungs, Mwambao Coastal Network, NEMC, TAFIRI, pamoja na viongozi kutoka wilaya za Kibiti, Rufiji, Mafia, Bagamoyo na maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Seleboni Mushi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, alisema mikoko ni rasilimali ya kipekee inayosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda viumbe wa baharini, na kuimarisha usalama wa chakula.

“Mikoko ni ngome dhidi ya dhoruba, hifadhi ya kaboni, chanzo cha kipato, na hifadhi ya viumbe hai. Inalinda maisha ya pwani na kutoa ajira kwa jamii,” alisema Mushi.

Aliongeza kuwa licha ya faida hizo, mifumo ya mikoko inaendelea kukumbwa na changamoto kubwa zikiwemo uvamizi wa ardhi, ukataji miti hovyo, na ujenzi holela – hali inayotishia uhai wake.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka TFS, Salehe Beleko, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi Prof. Dos Santos Silayo, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwani ni mara ya kwanza Tanzania kuadhimisha Siku ya Mikoko Duniani kitaifa kwa kiwango kikubwa.

“Ni tukio la kihistoria. TFS tunalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa, na tayari kesho tutazindua rasmi Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi na Uendelezaji wa Mikoko katika hoteli ya Protea,” alisema.

Beleko alibainisha kuwa mikoko ni sehemu ya urithi wa taifa na inahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, wadau na jamii ili kuhakikisha inalindwa ipasavyo.

Mhe. Mtambule alitumia jukwaa hilo kuwaagiza wenyeviti wa mitaa iliyopo kwenye fukwe za bahari kama Mbweni Maputo, Kunduchi Mtongani, Bweni Taita, Malindi, Mbezi Beach A na B, na wengine, kuchukua hatua kali dhidi ya uharibifu wa maeneo ya mikoko, ikiwemo ukataji haramu wa miti na ujenzi holela.

“Tutumie sheria zilizopo. TFS washirikiane na serikali za mitaa kufanya doria za mara kwa mara. Kubomoa ni rahisi, kujenga ni kazi,” alisisitiza.

Mratibu wa Mipango ya Bahari kutoka WWF, Dkt. Modesta Medard, alieleza kufurahishwa na mchango wa TFS katika kulinda mazingira na kuitaja taasisi hiyo kama jeshi maalum la ulinzi wa mazingira nchini.

“TFS ni mfano wa taasisi ya serikali inayoishi kwa vitendo. Tupo tayari kuendelea kushirikiana nanyi,” alisema Dkt. Medard.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...