Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)pamoja na wadau wa uihifadhi nchini wamepanda miti ya mikoko na kufanya usafi wa fukwe huku viongozi wa serikali za mitaa na wananchi wakihimizwa kutunza mikoko iliyopo katika maeneo mbalimbali.

Upandaji wa miti ya mikoko na usafi wa fukwe umefanyika leo Agosti 4,2025 eneo la Kilongawima wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani ambapo TFS kwa kushirikiana na wadau hao wamepanda miti 1000 ya mikoko katika eneo hilo kati ya miti 5000 itakayopandwa katika maadhimisho hayo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule ametumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa kulinda na kutunza miti ya mikoko na yeyote ambaye atabainika kuiharibu hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Tuna kıla sababu kuhakikisha tunashirikiana na TFS na wadau wengine wa uihifadhi na ni jukumu letu sote kuhakikisha tunaendelea kutunza mikoko na kuhakikisha tunaipanda.Leo hii tumepanda miti 1000 kati ya miti 5000 ambayo tutapanda katika maadhimisho ya siku ya mikoko duniani.

“Nitoe maelekezo kwa viongozi wetu wa Serikali za mitaa na watendaji wa kata katika Wilaya hii ya Kinondoni kwa kushirikiana na wananchi wote hasa maeneo ambayo kuna miti ya mikoko tushirikiane kuitunza na kuilinda.

“Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi kujiangalia tu wao wenyewe na ndio wamekuwa wakiharibu miti ya mikoko kwa kuikata kwa ajili ya shughuli mbalimbali na wanaofanya hivyo hawajui faida ya uwepo wa miti hiyo.”

“Niwaombe TFS kusaidia katika kufanya doria za kutosha kwenye hayo maeneo na tunapombaini mtu yeyote akiwa anafanya shughuli za kijamii ,shughuli za maendeleo maana kuna wengine wanakata hiyo mikoko kujenga nyumba kwenye hayo maeneo na wengine kufanyashughuli nyingine tuchukue hatua maana kubomoa ni rahisi kujenga ni kazi

Kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya mikoko duniani amesema inasema hivi ;Linda mikoko kwa ustawi wa maisha ya sasa na yajayo na hivyo amesisitiza umuhimu wa wadau wa uhifadhi kuwa kitu kimoja katika kulinda miti ya mikoko pamoja na aridhi oevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Misitu Wizara ya Maliasili na Utalii Celebone Mushi amesema kwa sasa nusu ya mikoko duniani inatoweka hivyo ni muhimu kuhakikisha wadau pamoja na wananchi kushirikana kuitunza.

“Hifadhi ya misitu ya mikoko ni hifadhi kwa ajili ya viumbe hai ,inasaidia jamii hasa Pwani katika kujipatia kipato ,lakini husaidia kuhifadhi fukwe kutokana na dhuruba za bahari lakini hifadhi hizo husaidia kuhifadhi cabon kwa maneno mengine misitu ya mikoko inasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi .

“Kwaupande wa Tanzania Bara hifadhi ya mikoko ni takriban hekta 158000 na zimeenea katika mikoa ambayo ni ukanda wa Pwani .Hata hivyo bado kunachangamoto nyingi ambazo zinaikabili misitu ya Ikolojia hii ambazo ni pamoja na uvamizi.

“Tafiti zinaonesha katika miaka 40 hivi nusu ya mikoko duniani inaonekana inatoweka na hiyo ni tishiokwa mazingira na uchumi,ni tishio kwa kuwa na mabadiliko ya tabianchi,”amesema na kusisitiza hivyo juhudi hizo za wadau ni sehemu ya kuhakikisha hifadhi za mikoko zinaendelezwa

Pia amesema juhudi hizo zinazofanywa na wadau ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ni mhifadhi namba moja na moja ya maelekezo yake ni kuhakikisha hifadhi zote zinatunzwa na zinahifadhiwa ipasavyo.

Wakati huo huo Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi Tanzania kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Naibu Kamishna wa Uhifadhi Salehe Beleko amewashukuru wadau wote kwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambayo ni ya kwanza kufanya nchini .

“Tunawashukuru wadau wote kwa kuwepo hapa leo hii sisi TFS tumekasimishwa tu kusimamia rasilimali za misitu ,misitu hii ni mali ya jamii na uwepo wenu unatupa moyo kwani inaonesha hatuko peke yetu.”

Amesisitiza mikoko ni maisha, mikoko ni uchumi na kubwa zaidi mikoko inaimarisha mazingira na kuongeza jambo la msingi ni kuhakikisha elimu ya faida za mikoko inaendelea kutolewa kwa wananchi.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...