Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kuwa Serikali inakwenda kuifungua Korogwe kwa barabara za lami.

Ametoa kauli hiyo leo Septemba 30,2025 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo ametumia nafasi hiyo mbali ya kuomba kura kuzungumzia ujenzi wa miundombinu ya barabara.

“Kuna kiu kubwa ya miundombinu ya barabara tutazidi kuifungua korogwe kwa lami na njia tutakayoanza nayo ni Soni - Bumbuli - Dindira - Korogwe kilometa 74 na barabara ya Old Korogwe - Kwa mndolwa - Magoma - Mashewa - Bombo Mtoni - Mabokweni kilometa 128 hizo tunakwenda kuzijenga kwa kiwango cha lami.”

Pia Dk.Samia amesema kwamba Serikali katika miaka mitano ijayo itaendelea kukamilisha utekelezaji wa barabara ya Manundu ambayo wanakwenda kuiangalia kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) au TANROADs kuona kama wanaweza kuitengeneza.”Tutakwenda kuiangalia barabara hiyo.”

Wakati huo huo Dk.Samia amesema ndani ya Korogwe kunapita mradi mkubwa wa kitaifa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Chongoleani.

“Kwahiyo hapa tunakwenda kujitahidi mradi ukamilike tukijua kwamba korogwe ni kituo muhimu kwani kuna ajira zitapatikana kupitia mradi huo.”

Pamoja na hayo amesema Serikali hatujasahau pendekezo la kuanzishwa bandari kavu katika Old Korogwe na hiyo ni kwa ajili ya kuondoa msongamano wa magari katika bandari ya Tanga ambako shughuli zimeongezeka kutokana na maboresho waliyoyafanya.

Katika hatua nyingine mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu na wanapochagua wachague mgombea Urais kupitia CCM ambaye ni yeye, wabunge na madiwani ili wakaendeleae kutekeleza miradi ya maendeleo.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...