Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Tanga

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza Taifa, amedhamiria kurejesha hadhi ya mkoa huo kuwa wa viwanda.

Ametoa kauli hiyo leo Septemba 29,2025 alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano huo uliofanyika katika Uiwanja vya Usagara mkoani Tanga ambapo ameeleza kwa kina mipango ya Serikali ya kwa miaka mitano ijayo katika Mkoa huo.

Dk. Samia ametangaza  mikakati kujenga reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 1,108 kutoka Tanga - Arusha hadi Musoma ambayo itaunganishwa na Bandari ya Tanga.

"Tutaanza utekelezaji mradi wa reli kuunganisha Bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musoma takriban kilometa 1,108. Reli hii itafungua maeneo ya viwanda na madini hivyo kuongeza fursa za ajira ndani ya Mkoa wa Tanga.”i

Amesema reli hiyo ni sehemu ya mpango wa maboresho ya Bandari ya Tanga kuwa eneo maalum la bohari ya mafuta na gesi.

"Bandari ya Tanga inakwenda na maamuzi tuliyoyafanya kuwa Tanga ni bohari ya mafuta na gesi, hilo litachangia kuzalisha ajira nyingine 2,100. Hili linakwenda kunyanyua uchumi wa wanatanga.

"Mbali na mradi huu, tuna mradi mwingine wa kimkakati inayofungamana na bandari hii. Moja wapo ni mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani.

“Mradi ambao umekamilika kwa asilimia 84 na umeleta manufaa mengi sana kwa mfano tayari eneo la Chongoleani pekee watu 1,300 wameajiriwa kwenye mradi huu na ndani ya Wilaya ya Tanga watu 2,000 wameajiriwa."

Mbali na ujenzi huo,  amesema  Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) zitashirikiana kujenga barabara ya Handeni - Singida.

"Barabara ya Handeni - Singida hii nayo tumeiunganisha kwa sababu watakaojenga bandari ni wenyewe TPA kwa sababu ya urahisi kusafirisha mizigo yao. TANROADS watashirikiana na bandari kujenga barabara hiyo," amesema Dk. Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza pia  serikali itafanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa barabara ya Dar es Salaam - Chalinze - Segera - Arusha.

Katika  kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda amesema serikali imevutia wawekezaji watakaojenga kiwanda cha kuunganisha magari ya wagonjwa.

"Mtupe kazi, tukafanyekazi tujenge utu wa Mtanzania. Tujenge utu wa mwana Tanga kwa sababu ukiimarisha huduma ya maji, afya, elimu, umeme unaimarisha utu wa Mtanzania.

"Tunawaomba mchague Chama Cha Mapinduzi ili mfanyekazi, tuimarishe na tujenge utu wa Mtanzania," amesema Dk.Samia.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...