Tume ya Ushindani (FCC) na Tume ya Ushindani wa Haki Zanzibar (ZFCC) zimetia saini mkataba wa ushirikiano wenye lengo la kuhakikisha masoko yanakuwa na ushindani wa haki na kulinda maslahi ya walaji katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Dkt. Hashil Abdalah, alisema makubaliano hayo yameweka misingi muhimu ambayo pande zote mbili zinapaswa kuizingatia katika utekelezaji.
“Kwanza, FCC na ZFCC zinapaswa kuteua watu au timu maalum kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya. Pia, ndani ya kipindi cha miezi mitatu—au hata chini ya mwezi mmoja—ni muhimu kutengeneza nyaraka kama ‘roadmap’ au ‘plan of action’ zitakazotuongoza katika utekelezaji,” alisema Dkt. Hashil.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupanga muda wa utekelezaji wa kila jukumu. “Kitu kisipopangiwa muda mara nyingi hakitekelezeki. Tunapaswa kujua tunatekeleza nini na kwa muda gani, ili tukifika wakati husika tuweze kujitathmini,” aliongeza.
Dkt. Hashil pia alibainisha kuwa watumishi wa FCC na ZFCC wanapaswa kupatiwa mafunzo na semina elekezi ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu dhamira ya mashirikiano hayo. “Dhamira yetu ni kusimamia, kuratibu na kuwezesha biashara kwa mujibu wa falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambao wanasisitiza mazingira bora ya biashara,” alifafanua.
Vilevile, aliagiza kuwekwa mpango wa tathmini ya utekelezaji wa makubaliano hayo. “Tuwe na tathmini ya robo mwaka au nusu mwaka ili kuhakikisha yale tuliyopanga yanaendelea kutekelezeka kwa wakati,” alisema.
Dkt. Hashil alihitimisha kwa kusema kuwa utiaji saini huo ni hatua muhimu katika kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi na kusukuma mbele maendeleo ya viwanda na biashara.

“Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza nguvu na uwezo wa pamoja kukabiliana na changamoto za ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji, ambazo mara nyingi huathiri Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo utahusisha kubadilishana taarifa, mafunzo ya pamoja, ujenzi wa uwezo katika tafiti pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.
Bi. Ngasongwa alisisitiza kuwa makubaliano hayo yataimarisha uhusiano kati ya taasisi hizo na serikali zote mbili, na kuhakikisha kuwa masoko yanabaki kuwa ya haki, yenye ushindani na yenye kulinda maslahi ya walaji. Aliwashukuru wote waliofanikisha mchakato huo na kuwataka wadau kutumia fursa hiyo kuimarisha utendaji.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Bi. Aliyah Juma, alisema tume yao ipo tayari kushirikiana kwa karibu na FCC katika utekelezaji wa makubaliano hayo.
“Tunalenga kushughulikia changamoto zote zilizopo sokoni kwa pamoja ili kulinda ushindani wenye tija na haki kwa pande zote. Sisi kama ZFCC tuko bega kwa bega kuhakikisha kile kilicho kwenye makubaliano kinatekelezwa kwa weledi na ufanisi,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...