*Amhakikishia mgombea Urais Pwani watamchagua kwa kura nyingi za kihistoria
*Asema hawapo tayari kuchanganya pumba na mchele…kwani hawafanyi biashara hiyo
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Pwani.
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dk.Jakaya Kikwete amewaomba wananchi wa Mkoa wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kumpigia kura ya ndio mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwatumikia Watanzania.
Akizungumza mbele ya Dk.Samia akiwa katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025 Rais Mstaafu Kikwete amesema “ Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM karibu Pwani.
“Ni furaha iliyoje kuwa nawe tena mkoani kwetu.
Tulikuwa nawe Kwala wakati wa uzinduzi wa bandari kavu na wakati ule ulikuwa unatimiza majukumu yako ya nchi.Leo umekuja kuomba ridhaa ya wana Pwani tukuchague kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
“Lakini napenda kukuhakikishia mkoa wa Pwani utakuchagua wewe, utapata kura nyingi sana zisizokuwa na mfano wake katika historia ya mkoa wetu.”
Akizungumza zaidi Rais Mstaafu Kikwete tena hatua kwa hatua na kwa utulivu mkubwa amesema “Kwanni tutakuchagua?Maelezo ya wagombea ubunge wameeleza kwa ufasaha na wengine waliopo ungewapa nafasi wangesema kama walivyosema waliopata bahati ya kuzungumza.
“Umezikabili kwa mafanikio changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huu tena
umezikabili kwa ufanisi, kwa umakini na ujasiri mkubwa.Mcheza kwao hutuzwa ,umetutendea mema mengi ,umetutendea mazuri mengi “
“Niwajibu wetu sasa kukulipa mema.
Tutakulipa kwa wema uliotutendea tutapiga kura kwa wingi mpaka zifurike kwenye sanduku ka kura la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Lakini tunatambua umuhimu wa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kukupatia wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na bak uhakikishia kama Bunge linalomalizika sasa wabunge wote ni wa CCM na litakalokuja kutoka Pwani wabunge wote ni wa CCM na ninaamini kwa nchi nzima itakuwa hivyo
“Pia tutakuletea madiwani wa Chama Cha Mapnduzi ili halmashauri za Wilaya na Miji zote ziwe chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi. Hatupo tayari mheshimiwa Rais na mgombea wetu kuchanganya pumba na mchele…
“Hatufanyi biashara ya namna hiyo,tunayajua madhara yake na hatutathubutu kufanya hivyo ndio maana tunasema Oktoba tunatiki mara tatu kwako rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge na Madiwani
“Mwisho nikupe pole na hongera kwa kampeni umechanja mbuga kweli kweli ulianzia Dar es Salaam ,ukaja Morogoro …mpaka nashindwa kusema ukaenda Lindi na Mtwara ndio umekuja hapa.Nikwambie unaonekana unaafya njema.
“Naamini utamaliza salama tunakuombea umalize salama tena kwa ushindi mkubwa ili Watanzania waendelee kunufaika na uongozi wako.Umeiongoza nchi yetu vizuri wewe ni mama mwema unajali changamoto za wananchi unaowaongoza na mwepesi kuchukua hatua.
“Kama zilivyoelezwa na waliotangulia
nchi yetu ina umoja nchi yenye makabila 120 wa rangi mbalimbali waumini wa dini mbalimbali lakini hakuna ugomvi wa kabila,hakuna ugomvi wa kidini wala hakuna ugomvi wa maeneo.
“Muungano wetu ni imara na bado ni wa kupigiwa mfano barani Afrika na nchi nyingine.Tunashukuru nchi ni tulivu maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanapatikana na yanaonekana na una maono mazuri kwa miaka mitano ijayo mpaka miaka 25 inayofuata
“Kwahiyo nakuombea tena kwa Wana Pwani tuchague CCM tumchague Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuongoza .Wamekuhakikishia wenyewe tutakupigia kura tena za kishindo kikubwa.”amehitimisha Kikwete huku akisisitiza Oktoba 29 Tunatiki Tunatiki Tunatiki kwa Samia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...