Na Mwandishi Wetu, Anjouan Comoro

BALOZI wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu, amewahakikishia wananchi wa Visiwa vya Comoro kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana nao katika sekta ya afya, hususan katika utoaji wa huduma za kibingwa, mafunzo kwa wataalamu wa afya, na uratibu wa rufaa za wagonjwa wanaohitaji matibabu maalum nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Kambi Maalum ya Matibabu ya Kibingwa iliyofanyika katika Hospitali ya Bambao, Anjouan, Balozi Yakubu alisema Serikali ya Tanzania itaendeleza jitihada za kuimarisha urafiki na ushirikiano wa afya kati ya mataifa hayo mawili kwa lengo la kuinua ubora wa huduma za afya kwa wananchi wa Comoro.

“Urafiki wetu na Comoro umejengwa katika misingi ya utu, taaluma na dhamira ya pamoja ya kuhudumia binadamu,” alisema Balozi Yakubu.

“Tanzania itaendelea kushirikiana na Comoro katika kujenga mifumo imara ya afya kwa manufaa ya wananchi wetu wote.” alisema

Alisema wagonjwa 3,653 wamepatiwa huduma, 20 wafanyiwa upasuaji muhimu

Na kwamba kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kambi hiyo, jumla ya wagonjwa 3,653 walipata huduma za matibabu ya kibingwa katika hospitali za Hombo, Bambao na Pomoni.

Alisema wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa kuokoa maisha.

Takwimu hizo zilitolewa katika taarifa ya mwisho ya kambi hiyo, iliyotekelezwa chini ya uratibu wa Global Medicare kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Visiwa vya Komoro.

Kambi hiyo maalum ilihusisha madaktari bingwa 52 kutoka hospitali kuu za taifa, ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD)

Gavana wa Anjouan: Ziara Tanzania Januari 2026

Gavana wa Kisiwa cha Anjouan, Dkt. Zaidou Youssouf, akiwa ameambatana na Mshauri wa Rais wa Komoro anayeshughulikia masuala ya siasa, Humed Msaidie, walieleza kufurahishwa na ubora wa huduma zilizotolewa na timu ya madaktari kutoka Tanzania.

Aidha, walitangaza kuwa watafanya ziara rasmi nchini Tanzania mwezi Januari 2026 kwa lengo la kukamilisha makubaliano ya ushirikiano wa afya, ikiwemo kuimarisha mfumo wa rufaa za wagonjwa wa Komoro wanaohitaji matibabu ya kibingwa katika hospitali za Tanzania.

Wizara ya Afya Tanzania yatoa kipaumbele kwa mafunzo na vifaa tiba

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Asha Mahita, ambaye pia ni Mratibu wa Taifa wa Tiba Utalii, alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaweka mkazo katika maeneo ya mafunzo kwa wataalamu wa afya, usambazaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na ubadilishanaji wa teknolojia na utaalamu kati ya Tanzania na Comoro.

“Ushirikiano huu ni fursa ya kubadilishana ujuzi, teknolojia na uzoefu wa kitabibu kwa manufaa ya mataifa yote mawili,” alisema Dkt. Mahita.

Kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa, iliyofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 11 Oktoba 2025, imeweka alama ya kipekee katika Diplomasia ya Afya kati ya Tanzania na Comoro, ikionesha dhamira ya Tanzania katika kusaidia mataifa jirani kupitia huduma za afya bora, elimu, na mafunzo ya kitaalamu.

Zaidi ya wagonjwa elfu tatu walihudumiwa kwa moyo wa upendo na weledi, jambo lililowagusa wananchi wa Komoro na kuimarisha uhusiano wa kindugu kati ya nchi hizi mbili.

“Kazi hii imeacha alama katika mioyo ya wananchi wa Anjouan,” ilielezwa katika taarifa ya mwisho ya kambi hiyo. “Tanzania imeonesha mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma za afya barani Afrika.”






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...