Na Emmanuel Mbatilo, Michuzi Tv

Bei ya mazao ya nafaka ikiwemo mchele na maharage katika Soko la Mbagala Rangi Tatu, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, imeendelea kupanda kwa kasi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, hali iliyoongeza ugumu wa maisha kwa wananchi hususan wenye kipato cha chini.

Kwa sasa, kilo moja ya mchele inauzwa kati ya Sh. 2,300 hadi Sh. 3,000 kulingana na ubora, kutoka wastani wa Sh. 1,800 hadi Sh. 2,000 mwezi Julai mwaka huu.

Aidha, bei ya kilo ya maharage imepanda mpaka kufikia Sh. 3,500 hadi Sh. 4,000, ikilinganishwa na Sh. 2,800 hadi Sh. 3,200 za miezi ya nyuma.

Wafanyabiashara sokoni hapo wanasema kupanda kwa bei kumetokana na kuanza kwa msimu wa kilimo 2025/26, hali inayosababisha upatikanaji mdogo wa nafaka sokoni, kwa kuwa wanunuzi wa kati (middlemen) wameanza kununua kwa wingi mashambani kusubiri mavuno yajayo.

Akizungumza na Michuzi Media, Agness Mushi, mmoja wa wauzaji wa nafaka sokoni hapo amesema biashara zao zimeyumba kutokana na wananchi kupunguza ununuzi.

“Kwa sasa wateja ni wachache sana. Watu wanakuja wakiulizia bei lakini wengi wanaondoka bila kununua. Tunalazimika kukaa na mzigo muda mrefu kuliko ilivyokuwa mwezi wa saba na wa nane. Bei imepanda na hali ya uchumi kwa wananchi sio nzuri,” amesema Agness.

Naye Hassan Juma, muuzaji wa mchele, amesema gharama za usafirishaji kutoka mikoani zimechangia kuongeza bei ya bidhaa hizo.

“Kutoka Songea na Mbeya usafiri nao umekuwa juu, mafuta yamepanda, lakini huku sokoni tunabaki kulaumiwa. Wateja hawaelewi kwamba gharama zinaanzia shambani na barabarani kabla mzigo kufika hapa,” alisema.

Baadhi ya wananchi waliofika sokoni hapo wameonesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa maisha endapo bei hizo zitaendelea kupanda.

“Kila siku bei zinapanda, mishahara haiongezeki. Hata ugali na Maharage sasa imekuwa taabu. Hatujui tutafika wapi,” amesema Rehema Ally, mkazi wa Mbagala Chamazi.

Kwa sasa wakulima katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na Katavi wanaendelea kuandaa mashamba kwa msimu wa kilimo 2025/26, hali inayoonekana kuathiri ugavi wa nafaka katika masoko ya jijini Dar es Salaam, ikiwemo Mbagala, Buguruni, Kariakoo na Tandale.

Wafanyabiashara wameiomba Serikali kushirikiana kwa karibu na wakulima pamoja na wasafirishaji ili kudhibiti upandaji holela wa bei na kuhakikisha upatikanaji wa nafaka kwa gharama nafuu wakati wakisubiri mavuno mapya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...