Benki ya Stanbic leo (ijumaa) imekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 60 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kusaidia kuboresha huduma za afya nchini.
Msaada huo, unaojumuisha kompyuta, vitanda, viti vya wagonjwa (wheelchairs), matoroli na vifaa vya usafi, ulikabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Stanbic Bank, Bw. Omari Mtiga, kwa niaba ya benki hiyo, na kupokelewa na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Amani Malima.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Bw. Mtiga alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango endelevu wa uwajibikaji wa kijamii wa Stanbic Bank unaolenga kurudisha fadhila kwa jamii, sambamba na maadhimisho ya Miaka 30 ya Kukua Pamoja tangu benki hiyo ianze kutoa huduma nchini Tanzania.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu, tunalenga kusaidia hospitali kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa watoa huduma. Hii ni moja ya njia tunazosherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania,” alisema Bw. Mtiga.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirya Ukio, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka, kwani hospitali inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa baadhi ya vifaa muhimu. Tunawashukuru Stanbic Bank kwa moyo huu wa kizalendo,” alisema Dk. Ukio.
Hafla hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, inayoongozwa na kaulimbiu 'Mission Possible', ambapo wafanyakazi wa Stanbic Bank walijitolea pia kufanya usafi katika baadhi ya maeneo ya hospitali kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.
Mkuu wa kitengo cha wateja binafsi na wateja maalum wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga (mwenye fulana ya bluu) akipeana mkono na Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Dkt. Amani Malima wakati wa makadhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 60 kutoka ya benki ya Stanbic, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja na pia sehemu ya benki hiyo kuadhimisha miaka 30 ya kutoa huduma nchini.Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya Stanbic, Mariam Maumba akiongoza wafanyakazi wa benki hiyo kwenye zoezi la kufanya usafi katika Hospitali ya Rufaa Tumbi Kibaha mkoa wa Pwani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ambapo pia walitoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 60 katika hospitali hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...