Katika kuadhimisha miaka tisa ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake, HaloPesa, kampuni inayoongoza katika huduma za kifedha kwa njia ya simu nchini Tanzania, imetoa mchango wa viti mjongeo 15 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala. Mchango huu ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kusaidia sekta ya afya na kuimarisha ustawi wa jamii.
Akizungumza wakati wa tukio la makabidhiano, Mkurugenzi Mkuu wa HaloPesa, Bw. Nghiem Anh Thong, alisema:
“Tunajivunia kuadhimisha miaka 9 ya kutoa huduma bora za kifedha kwa mamilioni ya Watanzania. Mafanikio haya si ya kibiashara pekee bali pia ni nafasi ya kutambua wajibu wetu wa kijamii. Mchango huu wa viti Mjongeo ni ishara ya dhamira yetu ya kuunga mkono sekta ya afya na kuboresha maisha ya wagonjwa wenye uhitaji maalum.”
Katika hafla hiyo, Bw. Thong alimkabidhi rasmi viti hivyo kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dkt. Aileen Barongo, kuashiria ushirikiano thabiti kati ya sekta binafsi na huduma za afya za umma.
Naibu Mkurugenzi wa HaloPesa, Bw. Magesa Wandwi, aliongeza:
“Miaka 9 ya HaloPesa ni ushahidi wa uhusiano wetu wa karibu na jamii. Tunaamini mafanikio halisi hupatikana pale tunapochangia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Msaada huu si wa kifedha tu, bali ni ujumbe wa mshikamano na dhamira ya kweli ya kujenga jamii bora.”
Kwa upande wa masoko, Afisa Masoko wa HaloPesa, Bi. Aidat Lwiza, alisisitiza:
“HaloPesa si tu huduma ya kifedha, bali ni taasisi inayowekeza katika ustawi wa jamii. Tunaamini mafanikio ya biashara yana thamani zaidi yanapoambatana na matokeo chanya kwa jamii. Viti hivi mjongeo vitasaidia sana wagonjwa wenye changamoto za kutembea.”
Kwa niaba ya Hospitali ya Mwananyamala, Dkt. Aileen Barongo alitoa shkrani zake:
“Tunatoa pongezi za dhati kwa HaloPesa kwa mchango huu muhimu. Katika mazingira yenye uhitaji mkubwa wa vifaa tiba, msaada huu wa viti mjongeo utaboresha kwa kiasi kikubwa huduma kwa wagonjwa. Tunathamini ushirikiano huu na tunatarajia kuendelezwa kwa manufaa ya wote.”
Katika kuhitimisha, HaloPesa imetoa wito kwa taasisi na wadau wengine wa sekta binafsi kutembelea vituo vya afya na kuangalia maeneo yenye uhitaji ili kuchangia kwa moyo wa kujitolea. Msaada wa aina yoyote unaweza kuleta tofauti kubwa katika maisha ya wananchi, hasa wale walioko katika mazingira magumu.
“Tunaamini kila shirika lina nafasi ya kuchangia ustawi wa jamii. Tunawahamasisha wengine kuiga mfano huu – kushirikiana kwa pamoja ili kujenga taifa lenye afya bora na mshikamano wa kweli,” alihitimisha Bi Aidat Lwiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...