NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
WANAWAKE wa Kata ya Gongo la Mboto wamehamasishwa kushiriki katika nafasi za uongozi na kujiimarisha kiuchumi kupitia Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) baada ya kufanya tathimini ya mradi wa Women’s Leadership and Economic Rights (WLER) unaoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na UNWOMEN
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24, 2025 Jijini Dar es Salaam, Muweka Hazina wa Kituo Cha Taarifa na Maarifa cha kata hiyo, Bi. Hajra Mbwambo amesema kufanya tathimini kumewapa nguvu ya kuibua na kuwaandaa wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii badala ya kubaki nyuma kwa hofu au utegemezi.
“Wanawake wengi tulikuwa tunajiona hatuwezi. Kufanya tathimini imetusaidia kujitambua na sasa wengi wameingia kwenye biashara, licha ya kuwa mitaji ni midogo,” amesema.
Hata hivyo, alitaja urusimu katika upatikanaji wa mikopo kama kikwazo kinachowakatisha tamaa wanawake wanaotaka kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa kituo hicho, Bw. Humphrey Mgeta, amesema waliendesha uhamasishaji kupitia makundi ya bodaboda, wanafunzi na akinamama ili kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi.
“Awali wanawake walikuwa waoga kugombea au hata kupiga kura kwa maamuzi yao, lakini sasa tunayaona matokeo. Ushawishi umeanza kuzaa viongozi wanawake katika ngazi ya jamii,” amesisitiza.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana nchini Tanzania yakiwemo kuchaguliwa kwa Rais mwanamke kwa mara ya kwanza wanawake wengi bado wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na mfumo dume, umaskini, na ubaguzi wa kijinsia.
Ukatili wa kijinsia kama ndoa za utotoni na mimba za utotoni zinaendelea kuwa kikwazo kwa elimu ya wasichana, jambo linalowazuia wanawake kupata fursa za kiuchumi na nafasi za uongozi katika jamii.
Wanawake, hasa wanaoishi vijijini, wanakumbwa na changamoto za kumiliki ardhi, kupata mikopo, mafunzo ya ujuzi na teknolojia, huku majukumu ya kazi zisizolipwa za malezi yakipunguza ushiriki wao katika maisha ya kijamii na kisiasa.
Katika kukabiliana na changamoto hizi, Mradi wa WLER umejikita katika kuimarisha ushiriki, uongozi, na haki za kiuchumi za wanawake na wasichana katika ngazi za jamii kwa kubadilisha mitazamo na desturi kandamizi za kijinsia.
Nae Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka TGNP Mtandao, Bi. Clara Godson amesema mradi wa WLER umejengwa juu ya mafanikio ya miradi ya awali na tayari umechangia mabadiliko kwenye jamii.
“Tunaona serikali za mitaa zikipanga bajeti zinazoangalia masuala ya kijinsia, huduma kwa watu wenye ulemavu zimeongezeka, na ajenda za usawa wa kijinsia sasa zinajadiliwa kwenye mipango ya maendeleo,” amesema.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...