Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili ( MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa, akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 27,2025 Dar es Salaam. wakati wa ziara ya kuangalia utekelezaji wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi HEET unaoendelea katika Kampasi ya Mloganzila..jpeg)
Mratibu wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi HEET, Profesa Erasto Mbugi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Oktoba 27,2025 Dar es Salaam. wakati wa ziara ya kuangalia utekelezaji wa mradi huo wa HEET unaoendelea katika Kampasi ya Mloganzila.
Sehemu ya ujenzi wa ya mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi HEET, inavyoonekana
Sehemu ya ujenzi wa ya mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi HEET, inavyoonekanaNa Karama Kenyunko Michuzi Tv
UDAHILI wa wanafunzi wa fani za afya katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) unatarajiwa kuongezeka kutoka wanafunzi 350 hadi 1,000 kufuatia utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaoendelea katika Kampasi za Mloganzila na Kigoma
Mradi huo unaojulikana kwa jina la HEET wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 120 unatarajiwa kumalizika mwezi Juni 2026 na kwenda kuwa suluhu ya upatikanaji wa wataalamu wa kibingwa wa utoaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kuimarisha Sekta hiyo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema hayo leo Oktoba 27, 2026 wakati wa ziara ya kuangalia utekelezaji wa mradi huo, Mloganzila Dar es Salaam
Amesema ongezeko hilo la udahili litachochewa na ujenzi wa Ndaki ya Tiba na miundombinu ya kisasa inayojengwa kupitia mradi huo, ambao unalenga kuboresha elimu ya juu nchini, hasa katika sekta ya afya na maendeleo ya kiuchumi.
“Takwimu zinaonyesha mwaka huu kati ya waombaji 31,026 waliokidhi vigezo, ni wanafunzi 986 pekee waliopata nafasi MUHAS. Kukamilika kwa mradi huu kutapunguza changamoto hiyo na kuongeza fursa kwa vijana wengi wenye sifa,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Amesema kuwa, Miundombinu mipya itajumuisha maabara 83 kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1400 bwalo la chakula, bweni la wanafunzi 320 na miundombinu ya TEHAMA itakayoboreshwa kwa kiwango cha juu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Profesa Kamuhabwa
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utawezesha chuo hicho kuongeza idadi ya wataalamu wa afya katika ngazi za Uzamili na Uzamivu, sambamba na kuimarisha utoaji wa huduma za tiba.
Aidha, Profesa Kamuhabwa ameongeza kuwa mradi huo utazalisha zaidi ya ajira 300 mpya katika hatua za ujenzi na baada ya kukamilika, kupitia nafasi za wahadhiri, watumishi wa afya na wataalamu wa kiufundi.
“Mradi huu si tu unakuza elimu na huduma za afya, bali pia unachochea uchumi kwa kununua vifaa na huduma kutoka kwa wazalishaji wa ndani,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Profesa Kamuhabwa, miundombinu ya tiba itakayojengwa itachochea utalii tiba (medical tourism) kupitia Kituo cha Moyo na Figo pamoja na Kituo cha Saratani ya Shingo ya Kizazi (Kigoma), hatua itakayopunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuongeza mapato ya taifa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Profesa Erasto Mbugi, amesema mradi umefikia asilimia 50 ya utekelezaji, huku serikali ikiendelea kuwezesha uboreshaji wa huduma za afya na fursa za ajira.
“Ujenzi huu utakamilika madaktari wetu watakuwa na uwezo wa kujifunzia hatua zote za tiba ndani ya nchi badala ya kwenda nje, jambo litakalopunguza gharama na kuongeza ubora wa mafunzo,” amesema Profesa Mbugi.
Ameongeza kuwa bado kuna mahitaji ya rasilimali fedha ili kukamilisha miundombinu iliyobaki na kupanua huduma kwa wananchi.
Naye, Yasinta Mkandawile, mkazi wa Mtaa wa Mpakani, Mloganzila, amesema ujenzi huo umeleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
“Vijana na wanawake wengi wamepata ajira kutokana na ujenzi huu. Tunaishukuru serikali kwa mradi huu kwani umefungua milango ya kipato na maendeleo katika jamii yetu,” amesema.



.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...