Mbeya, 13 Oktoba 2025
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limeimarisha ulinzi na usalama kwa kiwango cha juu kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, ambacho kinatarajiwa kufanyika kesho tarehe 14 Oktoba katika Jiji la Mbeya.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2025, Mwenge wa Uhuru umeingia rasmi katika Mkoa wa Mbeya ukitokea Mkoa wa Songwe, ambapo mapokezi yake yalifanyika kwa mafanikio makubwa katika mazingira ya utulivu na usalama, kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi wa Jiji la Mbeya.

Mpaka sasa, Mwenge huo umeshakimbizwa katika wilaya zote tano na halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya, na katika maeneo yote hayo hali ya usalama imeendelea kuimarika kwa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali.

Shughuli za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zitahitimishwa rasmi kesho, 14 Oktoba 2025, jijini Mbeya, ambapo Mwenge utazimwa katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa kitaifa pamoja na wageni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Tukio hilo pia litaambatana na kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ametoa wito kwa wananchi wote wa Jiji la Mbeya kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha hali ya utulivu na usalama inadumishwa kabla, wakati na baada ya shughuli hiyo ya kitaifa. Aidha, amewataka watumiaji wa barabara kuwa waangalifu na kufuata sheria pamoja na maelekezo yatakayotolewa na askari Polisi, ili kuhakikisha misafara ya viongozi na wageni inasafiri salama bila usumbufu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewahakikishia wananchi kuwa limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wakati wote wa hafla hiyo na kwamba litaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaokiuka sheria kwa makusudi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...