Katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara, zaidi ya watu milioni 940 bado hawana upatikanaji wa uhakika wa umeme, na zaidi ya milioni 700 wanategemea nishati hatarishi kama kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia. Nchini Tanzania, zaidi ya nusu ya wananchi—takribani watu milioni 36—wanaishi bila umeme.
Jamii nyingi vijijini hulazimika kutumia vyanzo vya nishati vyenye madhara kama vile mafuta ya taa na kuni kwa ajili ya mwanga na kupikia, hali inayochangia changamoto nyingi katika maisha yao. Wanawake ndiyo wanaoathirika zaidi kwani hutumia muda mwingi kukusanya kuni na kuvuta moshi wenye sumu wakati wa kupika. Aidha, wengi wao hukosa chanzo cha kipato cha kudumu.
Ili kukabiliana na changamoto hii, taasisi ya Puma Energy Foundation ilishirikiana na Solar Sister, shirika linalowawezesha wanawake katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara kuanzisha biashara za kuuza taa za zinazotumia nishati ya jua na bidhaa nyingine za nishati safi kwenye jamii zao.
Tangu mwaka 2010, kupitia mfumo wake uliofanikiwa na kutambulika kimataifa, Solar Sister imetengeneza mtandao wa zaidi ya wajasiriamali wanawake 12,000 wanaojulikana kama Solar Sister Entrepreneurs, ambao wamefikia zaidi ya watu milioni 5.5 katika eneo hilo. Solar Sister huwapa mafunzo katika masuala kama vile masoko, uhasibu, mkakati mpango wa biashara, pamoja na ushauri na upatikanaji wa mikopo midogo. Pia, huhakikisha kuwa bidhaa za nishati ya jua wanazouza ni imara na zenye ubora wa hali ya juu. Nchini Tanzania, mpango huu umewanufaisha zaidi ya watu milioni 2.3 tangu ulipoanzishwa mwaka 2013.
Awamu ya kwanza ya ushirikiano wa Puma Energy Foundation na Solar Sister, ulioanza mwaka 2023, ilijikita katika Mpango wa Kukuza Biashara, mpango ambao umewezesha wanawake 579 nchini Tanzania kupata mafunzo na msaada wa kibiashara. Mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na upatikanaji wa teknolojia, kama vile simu janja, yamewapa nyenzo zaidi za kuongeza mauzo, kipato, na kufikia kaya nyingi zisizo na umeme kwa nishati safi.
Katika awamu ya pili ya ushirikiano huu, iliyoanza mwaka 2025, Solar Sister inalenga kuajiri na kuwafundisha wanawake 500 zaidi katika mikoa mitatu mipya nchini Tanzania, kuwapa wanawake 200 ujuzi wa biashara za kidijitali, na kuwawezesha kuuza bidhaa 16,000 za sola, zikiwemo majiko safi 2,000.
“Lengo si kuuza bidhaa za nishati pekee,” alisema Cesear Mloka, Mkurugenzi Mkaazi wa Solar Sister Tanzania. “Ni kuwawezesha wanawake kujiamini, uhuru wa kifedha, na sauti yenye kuheshimiwa katika familia na jamii zao.”
Mfano hai wa walionufaika na mpango huu ni Neema Ally, ambaye kwa miaka mingi alikuwa akifanya kazi ya kulima mashamba ya watu wengine katika mkoa wa Songwe, kusini mwa Tanzania, akipata kipato kidogo cha kutosheleza mahitaji ya familia yake. Alitamani siku moja kuwa na shamba lake mwenyewe, lakini hakuwa na rasilimali za kumtoa katika mzunguko wa umaskini.
Maisha yake yalibadilika alipojiunga na Solar Sister. Kupitia mafunzo na ushauri, alianza safari yake kama mjasiriamali wa bidhaa za nishati. Faida aliyopata kupitia biashara yake ya sola, Neema aliweza kukodisha ekari tano za ardhi na kulima mahindi. Leo, hafanyi kazi kwa watu wengine tena; anaendesha shamba lake, anatoa ajira kwa watu wengine katika jamii yake, na kuhakikisha watoto wake wanapata elimu.
Hadithi ya Neema inaonyesha jinsi upatikanaji wa nishati na ujasiriamali unavyoweza kufungua njia na kuleta heshima, uhuru wa kiuchumi, na maendeleo ya jamii.
Mfano mwingine ni kupitia kwa Bi. Theresia John Robert, anayeishi kijijini Kaskazini mwa Tanzania, aliwahi kuishi nyumba ya kupanga, akipata riziki kupitia shughuli za kuponda mawe kwa mikono. Kazi hiyo ilikuwa ngumu kwake, na ndoto zake za maisha bora zilionekana kuwa hafifu.
Mwaka 2017, alijiunga na Solar Sister na kuanza kuuza taa za sola na majiko safi. Mwanzoni alikuwa na aibu na hofu ya kuzungumza na wateja wapya, lakini kwa muda alijijengea ujasiri, akianza kuendesha baiskeli kwenda vijiji vya mbali na mara nyingine kuuza bidhaa zake zote kwa siku moja. Kupitia kipato chake, Bi. Theresia aliweza kujenga nyumba yake mwenyewe — jambo ambalo hapo awali alidhani haliwezekani.
Hadithi yake inaonyesha ujasiri na dhamira ya wanawake wajasiriamali ambao, wakipatiwa nyenzo sahihi, hawatoishia kupata riziki tu bali wanafanikiwa na kustawi.
Kupitia ushirikiano wake ulioimarishwa na Puma Energy Foundation, Solar Sister inalenga kuwafikia watu 85,000 nchini Tanzania kwa bidhaa za nishati jadidifu na zenye kiwango cha chini cha kaboni, hivyo kupunguza hewa chafuzi, kuboresha afya za kaya, na kuimarisha uthabiti wa tabianchi. Lakini manufaa ya mpango huu hayapo kwenye bidhaa pekee. Kwa kuwaweka wanawake katikati ya suluhisho, ushirikiano huu unakuza ujasiriamali, unajenga uhuru wa kifedha, na unaimarisha uongozi wa wanawake katika jamii za vijijini.
“Tunajitahidi kuboresha maisha na kuleta mabadiliko yenye tija katika jamii,” anasema Laura Fruehwald, Meneja wa Programu wa Puma Energy Foundation. “Kupitia ushirikiano huu, nishati siyo tu chombo cha matumizi ya kila siku, bali pia kichocheo cha uwezeshaji na maendeleo endelevu.”
Nchini Tanzania, Puma Energy inaenda sambamba na juhudi za taasisi ya Puma Energy Foundation kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za nishati safi ya kupikia zenye ubora wa hali ya juu na bei nafuu. Juhudi hizi zinachangia ajenda ya kupikia kwa nishati safi kwa kutoa mbadala salama na unaopatikana kwa urahisi kwa kaya nyingi nchini, hivyo kupunguza zaidi hatari za kiafya na athari za kimazingira. Kwa kuunganisha nguvu ya uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali inayotolewa na taasisi na dhamira ya kampuni ya kutoa suluhisho la bidhaa na huduma za nishati safi ya kupikia ya uhakika, ushirikiano huu unaunda njia jumuishi ya upatikanaji wa nishati endelevu na maisha bora.
Kwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali, ushirikiano huu unalenga kuleta mabadiliko ya kudumu kwa kutoa upatikanaji wa nishati safi, kukuza uchumi wa vijijini, na kujenga jamii zenye afya bora na ustahimilivu mkubwa nchini Tanzania.













Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...