Na Rahel Pallangyo, Dar es Salaam
WACHAMBUZI wa masuala ya siasa, diplomasia na maendeleo wamewataka vijana na wananchi kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii kwa busara, uangalifu na uzalendo, wakisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kuhusu ukweli wa taarifa wanazopokea na kusambaza, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Wito huo umetolewa Oktoba 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa “Wajibu wa Kidijitali kwa Amani ya Nchi Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi” uliofanyika katika ukumbi wa American Corner, Makumbusho ya Taifa. Mdahalo huo uliandaliwa kwa lengo la kujadili namna teknolojia na mitandao ya kijamii inaweza kutumika kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.

Akizungumza katika mjadala huo, mchambuzi wa masuala ya diplomasia na siasa, Abdulkarim Atik, alisema vijana wanayo nafasi kubwa katika kuamua mwelekeo wa taifa kupitia mitandao ya kijamii. Alisema ni muhimu kutathmini ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza kwa sababu taarifa zisizo sahihi zimekuwa chanzo cha taharuki, migawanyiko na uhasama katika jamii.

“Ikiwa vijana watatambua ukweli wa taarifa wanazopata, itawasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuchangia katika kulinda amani ya nchi, hususan kipindi cha uchaguzi,” alisema Atik.

“Mara nyingi propaganda hujificha katika sura ya habari. Tunapaswa kuwa makini tusitumike kueneza ajenda zinazolenga kugawa taifa.”

Kwa upande wake, mwandishi wa habari wa Crown Televisheni, Imani Luvanga, alisema mitandao ya kijamii si adui wa jamii kama wengi wanavyodhani, bali ni nyenzo muhimu ya mawasiliano, elimu na maendeleo, ikiwa itatumiwa kwa uangalifu.

“Tatizo siyo mitandao, bali ni namna watu wanavyoiendesha. Matumizi sahihi yanaweza kuleta manufaa makubwa, yakiwemo maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Luvanga.

“Vijana wanapaswa kujitambua wanapotumia mitandao hiyo—waelewe sababu ya kuitumia, aina ya taarifa wanazozingatia na faida wanazotarajia kupata.”

Luvanga alisisitiza kuwa mitandao inaweza kuwa daraja la fursa kwa vijana wanaojihusisha na ujasiriamali, ubunifu na uandishi wa habari, iwapo itatumika kwa kujenga badala ya kubomoa. Aliongeza kuwa jamii inapaswa kujifunza kutumia majukwaa hayo kuhamasisha amani na ushirikiano badala ya maneno ya chuki.

Mdau wa siasa na maendeleo, Reeves Ngalemwa, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha misingi ya uzalendo tangu utotoni, akisema ni msingi wa taifa lenye uthabiti katika zama za kidijitali. Kwa mujibu wake, kuandaa watoto kuwa wazalendo kunasaidia kizazi kipya kutambua lipi ni sahihi na lipi si sahihi katika taarifa zinazozunguka mitandaoni.

“Ni muhimu kuweka mazingira ya kuwaandaa watoto kujifunza uzalendo tangu wakiwa shule za msingi ili wakue wakiwa na mapenzi ya kweli kwa nchi yao,” alisema Ngalemwa.

“Tunapojenga kizazi chenye misingi imara ya uzalendo, tunajenga jamii inayotumia teknolojia kwa manufaa ya taifa, si kwa uharibifu.”

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya vyombo vya habari na mpiga picha maarufu, Issa Michuzi, alihimiza wananchi kuwa makini na taarifa zinazochochea chuki au migawanyiko, akibainisha kuwa propaganda zinaweza kuathiri umoja wa kitaifa endapo hazitachunguzwa kwa makini.

“Watu wanatakiwa kuangalia mambo kwa umakini. Propaganda inaweza kuwa nzuri au mbaya. Tumefika hapa si kwa bahati mbaya, ni matokeo ya kuruka hatua,” alisema Michuzi.

“Kila mmoja awe mlinzi wa taifa kwa kutathmini taarifa kabla ya kuzisambaza. Mitandao inaweza kujenga au kubomoa, inategemea namna tunavyotumia.”

Michuzi alionya kuwa kutokuwa makini katika kusambaza taarifa zisizo sahihi mitandaoni kunaweza kusababisha jamii kuingia katika migogoro isiyo ya lazima, na kusisitiza kuwa kila raia ana wajibu wa kulinda amani kwa vitendo, ikiwemo nidhamu ya kidijitali.

Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe, aliwataka vijana kuwa na ndoto zilizoegemea katika muktadha wa kitaifa, akisema maamuzi yao ya kisiasa na kijamii yanapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa. Alisisitiza umuhimu wa vijana kuwa na mtazamo mpana katika kuchambua matukio na taarifa wanazokutana nazo.

“Vijana wanahitaji msingi imara ili maamuzi yao yawe ya kusonga mbele badala ya kuumiza taifa,” alisema Msimbe.

“Tunapaswa kuwa na kizazi kinachofikiri kitaifa, si kizazi kinachoendeshwa na matukio ya muda mfupi kwenye mitandao.”

Mdahalo huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wachambuzi, Magid Mjengwa, ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wa mawasiliano ya kidijitali, wanabloga kutoka TBN, wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, wadau wa amani na waandishi wa habari.

Washiriki walikubaliana kuwa mitandao ya kijamii ni uhalisia usioweza kuepukika katika maisha ya sasa, hivyo ni muhimu kwa Watanzania wote—hasa vijana—kuijua na kuitumia kwa manufaa ya taifa.

Mdahalo ulihitimishwa kwa wito wa pamoja wa kuimarisha elimu ya habari (media literacy) na maadili ya kidijitali, sambamba na kujenga utamaduni wa kuthamini ukweli na amani.

“Tanzania ni nchi ya amani. Tunapaswa kuhakikisha mitandao inabaki kuwa chombo cha kuunganisha Watanzania, si kuwatenganisha,” alihitimisha Mjengwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...