Na Mwandishi Wetu
MTHIBITI Ubora wa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni, Paschalina Herman Msofeo amewataka wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari St. Mary’s kutambua kuwa safari ya mafanikio yao katika elimu na maisha bado inaendelea, huku akisisitiza umuhimu wa kujiamini, kufanya kazi kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika kila hatua.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 24 ya Kidato cha Nne, Msofeo alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora yenye viwango vya kimataifa.
“Dhima yangu kubwa leo ni kuwatunuku vijana wetu vyeti vya kuhitimu, lakini zaidi kuwahakikishia kuwa Serikali ina ari ya dhati ya kuhakikisha wanafunzi wa taifa hili wanapata elimu bora wanayostahili,” alisema.
Msofeo aliitumia fursa hiyo kumpongeza Hayati Dkt. Gertrude Rwakatare, mwanzilishi wa shule za St. Mary’s, kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya elimu nchini.
“Tuna kila sababu ya kumkumbuka Dkt. Rwakatare kwa uongozi wake thabiti na jitihada za kuanzisha shule hizi zenye ubora wa hali ya juu. Leo tunapoadhimisha mahafali haya, tuendelee kumuombea apumzike kwa amani,” aliongeza.
Aidha, aliwataka wahitimu kuchukulia hatua ya kufuzu Kidato cha Nne kama mwanzo wa safari nyingine ndefu ya kitaaluma na maisha, huku akiwahimiza kuwa na imani na uthubutu kama silaha ya mafanikio.
“Vijana wangu, huu ni mwanzo tu wa safari. Jiaminini na mkumbuke kuwa imani thabiti ndiyo inayoyafanya yasiyowezekana yawezekane. Mvae roho ya kujiamini kama alivyofanya mama yetu Dkt. Rwakatare,” alisema Msofeo, akiwatakia mafanikio mema katika mitihani yao itakayoanza Novemba 10, 2025.
Kwa upande mwingine, aliwapongeza walimu wa St. Mary’s kwa kazi kubwa ya kuandaa vijana hao, akibainisha kuwa ubora wa mwalimu hupimwa si tu kwa matokeo ya darasani, bali pia kwa uwezo wa mwanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha baada ya shule.
“Mwalimu bora ni yule anayetoa elimu itakayomsaidia mwanafunzi kupambana na changamoto za maisha na kukubalika katika jamii,” alisema.
Aliwapongeza pia wazazi kwa kujitolea na kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora, akisisitiza kuwa juhudi hizo hazitapotea bali zitazaa matunda kupitia mafanikio ya watoto wao.
“Mmewekeza sehemu sahihi. Endeleeni kuwaunga mkono watoto wenu katika safari zao za kitaaluma. Watawalipa kwa matokeo mazuri,” alisema Msofeo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za St. Mary’s, Humphrey Rwakatare, aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuendelea kuiamini shule hiyo na kuikabidhi jukumu la kuwalea na kuwaelimisha watoto wao.
“Ninawashukuru wazazi kwa imani yenu kwetu. Natoa ahadi kuwa tutaendelea kutoa elimu bora inayowaandaa vijana kukabiliana na majukumu ya maisha yao,” alisema.
Aliwatambua pia walimu na wafanyakazi wote wa shule hiyo kwa kujituma na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata huduma na elimu bora kila siku.
“Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru walimu wetu kwa kazi kubwa mnayoifanya kila siku kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” alisema.
Rwakatare alimalizia kwa kuwakaribisha wazazi na wageni wote kuendelea kushirikiana na shule hiyo, akisisitiza kuwa St. Mary’s itaendelea kuwa chaguo bora kwa mzazi anayethamini maendeleo ya mtoto wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...