NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
WAHITIMU wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala mtambuko ikiwemo kupinga vitendo vya rushwa, ukatili wa kijinsia, utoaji wa elimu jumuishi, lishe shuleni, na mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na maambukizi mapya ya VVU.
Wito huo umetolewa leo Desemba 5, 2025 wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omary, wakati wa mahafali ya 33 ya ADEM ambapo jumla ya wahitimu 785 wa kozi zaStashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu -DELMA, Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule - DSQA na Astashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu -CELMA wamehitimu.
Dkt. Omary amesema masuala hayo yakiwa hayapatiwi uzito unaostahili yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Ameongeza kuwa serikali inawategemea wahitimu hao kwa kuwa ujuzi walioupata ni muhimu kwa mustakabali wa elimu nchini.
“Mtakaporudi katika vituo vyenu vya kazi, hakikisheni mnashirikiana na uongozi wa ngazi zote pamoja na jumuiya za shule ili kuhakikisha shule zinafanya vizuri kitaaluma na katika nidhamu,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi na utoaji wa mafunzo, Dkt. Omary alisema Serikali kupitia wizara itaendelea kushirikiana na ADEM kupunguza changamoto hizo na, inapowezekana, kuondoa kabisa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, alisema wahitimu wote wa ngazi mbalimbali ni wataalam mahiri wanaohitajika katika sekta ya elimu, na mchango wao ni muhimu katika kukuza rasilimali watu.
“Hii inaonesha kuwa chuo kinaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kupitia uzalishaji wa wataalam wa uongozi na usimamizi wa elimu,” alisema.
Aidha, Dkt. Maulid alibainisha changamoto ya kukosekana kwa bajeti ya kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa viongozi wa elimu, wakiwemo walimu wakuu, wakuu wa shule, maafisa elimu ngazi ya kata hadi mkoa, wathibiti wa shule na viongozi waandamizi wa wizara.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, chuo kitaimarisha ushirikiano na taasisi binafsi pamoja na mashirika ya kimataifa ili kuongeza rasilimali fedha na kuendeleza mafunzo.
“Tutaongeza nguvu kupitia ushirikiano wa ‘Public Private Partnership’ na ‘Tanzania Investment Centre’ ili kubainisha wadau wanaoweza kuwekeza katika maeneo ya ardhi tunayomiliki,” alieleza.
Aidha, aliwasihi wahitimu kutumia maarifa waliyopata kuelimisha jamii kuhusu athari za uvunjifu wa amani, mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa uzalendo.
“Wahitimu wakasimamie ipasavyo maeneo yao kwa kutoa maarifa kwa walimu na wanafunzi ili watambue thamani ya amani, uzalendo na maadili,” alisema Dkt. Maulid.


















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...