Mwandishi wetu Endulen Ngorongoro.
Uhusiano kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na jamii inayoishi ndani ya eneo la hifadhi umeendelea kuimarika kufuatia ziara za Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Bw. Abdul-Razaq Badru katika vijiji mbalimbali vilivyoko tarafa ya Ngorongoro ambapo leo tarehe 20 Desemba,2025 ametembelea Kata ya Enduleni, wilayani Ngorongoro.
Akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Endulen Mhe. Elias Sakara Nagol, Kamishna Badru ameeleza kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Uongozi wa hifadhi ya Ngorongoro na jamii, pamoja na kukagua maboresho ya miundombinu ya maji inayotumika kwa matumizi ya wananchi, mifugo na wanyamapori.
Katika ziara hiyo Kamishna Badru amewaeleza wananchi wa vijiji vya Kata ya Enduleni kuwa Mamlaka inatekeleza Miradi ya Maji katika kata za Endulen, Kakesio, Olbalbal na maeneo mengine na aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi na utunzaji wa miradi hiyo ambayo inagharimu fedha za Serikali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Enduleni, Dkt. Elias Sakara Nagol, amempongeza Kamishna Badru na wasaidizi wake kwa kuendeleza uhusiano ya karibu na jamii inayoishi ndani kwa kuwatembelea mara kwa mara, kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii na kuahidi kuwa wananchi wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa kutunza na kulinda hifadhi kupitia programu ya uhifadhi shirikishi.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...