Rukwa
Mkoa wa Rukwa umeendelea kujikita kuwa kitovu kipya cha uchimbaji wa madini ya emerald nchini, huku Serikali na wadau wa sekta hiyo wakihimiza vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo la Mponda lililopo Wilaya ya Sumbawanga, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, amesema mkoa huo una utajiri mkubwa wa madini ya emerald ambayo ni miongoni mwa madini adimu duniani.
Amesema kuwa kampuni mbili, Trinity Company Limited ya Tanzania na kampuni nyingine kutoka India tayari zimeonesha dhamira ya kuwekeza kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.
Amefafanua kuwa emerald hutumika kwa mapambo na ina thamani kubwa katika masoko ya kimataifa, ambapo karati moja ya ubora wa chini huuzwa kwa wastani wa Dola za Marekani 100 (sawa na takribani Shilingi 246,000), huku yale yenye ubora wa juu yakifikia kati ya Dola za Kimarekani 5,000 hadi 10,000 kwa karati.
Mhandisi Kumburu ametoa wito kwa vijana kuwekeza na kuchangamkia fursa zinazofunguka, akibainisha kuwa zaidi ya wawekezaji 10 walijitokeza mwaka uliopita baada ya mafunzo yaliyotolewa na ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha, ameongeza kuwa eneo la hekta 13,000 limetengwa kwa ajili ya utoaji wa leseni za madini 700 kwa wachimbaji wadogo, sambamba na fursa nyingine za uchimbaji wa shaba na titanium ambazo pia zimeanza kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Leseni ya uchimbaji wa emerald katika eneo la Mponda, Wilayani Sumbawanga Liberatus Suleiman, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano na kueleza kuwa tayari wameshaanza kuandaa miundombinu muhimu kabla ya kuanza uchimbaji rasmi.
Ametoa rai kwa vijana kujiunga na sekta hiyo akisema mkoa wa Rukwa una fursa ambazo zinaweza kuwaibua mabilionea wapya.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Rukwa, Masie Mwambene, ameipongeza Serikali na kuitaka Tume ya Madini kuongeza kasi ya kutangaza fursa ili kuongeza uwekezaji, ajira na wataalam wa ndani.
Amesema mwamko wa vijana umeongezeka kutokana na elimu endelevu inayotolewa na wataalam wa madini mkoani humo.
Ameeleza kuwa maendeleo ya sekta ya madini hasa kwenye uchimbaji wa emerald yataleta manufaa mapana ikiwemo ajira, ujenzi wa miundombinu ya barabara, umeme pamoja na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji, akiwataka vijana kusomea masuala ya sayansi ili kuongeza ujuzi ndani ya sekta hiyo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...