Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (MB.), Akikabidhi hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, leo Desemba 30, 2025 Mkoani Pwani.


*Bagamoyo Yageuka Kitovu cha Uwekezaji Kupitia Eneo Maalum la Kiuchumi

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (MB.), amekabidhi hati na kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, sambamba na kutoa Taarifa ya Hali ya Uwekezaji Nchini kwa Mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Zinga, Bagamoyo leo Desemba 30, 2025 Prof. Mkumbo amesema matukio hayo mawili ni utekelezaji wa maono ya Serikali katika sekta ya uwekezaji na maendeleo, na ni sehemu ya kutafsiri Sera ya Taifa ya Uwekezaji, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na miongozo ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema makabidhiano ya hati kwa wawekezaji ni hatua ya kisheria na kiutawala inayotoa uhakika wa ardhi na haki za uwekezaji, sambamba na kuhakikisha matumizi ya ardhi ya Taifa yanazingatia tija, uwazi na maslahi ya wananchi.

Katika hafla hiyo, wawekezaji waliokabidhiwa hati na kuanza au kupanua uwekezaji wao Bagamoyo ni MCGA Auto Limited, Canary Industries Limited kupitia Bahari Pack, Grosso Engineering and Fabricators Limited, Jaribu Cashew Production Limited, pamoja na Novara Steel Global Limited na Shah Steel Global. Miradi hiyo inalenga kuunganisha magari, kuzalisha vifungashio vya chakula, kutengeneza vifaa vya kilimo na chuma, pamoja na kusindika mazao ya kilimo kwa ajili ya soko la ndani na nje.

Prof. Mkumbo amesema uwekezaji huo unaashiria mabilioni ya shilingi, uanzishwaji wa maelfu ya ajira, ongezeko la mapato ya Serikali na kuimarika kwa hadhi ya Tanzania kama kivutio salama cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika.

Akitoa taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2025, Waziri huyo amesema uwekezaji umeendelea kuimarika kutokana na mazingira bora ya kibiashara, miundombinu inayoboreshwa na utulivu wa kisiasa.

Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi Disemba 29, 2025, miradi iliyosajiliwa imeongezeka kutoka miradi 252 hadi miradi 915, huku mitaji inayotarajiwa kuwekeza ikiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 3.79 hadi Dola za Marekani bilioni 10.95.

Kwa mwaka 2025 pekee, TISEZA imesajili zaidi ya miradi 915 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10,954.08, inayotarajiwa kuzalisha ajira 161,678 katika sekta za viwanda, ujenzi na usafirishaji. Kati ya miradi hiyo, 284 inamilikiwa na Watanzania, 449 na wageni, huku 182 ikiwa ya ubia.

Ameeleza kuwa Tanzania ina jumla ya SEZ/EPZ 34, na kupitia programu ya EPZ/SEZ kwa mwaka 2025, zilisajiliwa miradi 20 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 243.17, inayotarajiwa kuzalisha ajira 4,822 na mauzo ya nje ya Dola za Marekani milioni 227.43.

Katika maboresho ya mazingira ya uwekezaji, Prof. Mkumbo amesema Serikali imeimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja, matumizi ya TEHAMA, utoaji wa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, uanzishwaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya kimkakati, pamoja na kuimarisha Benki ya Ardhi yenye zaidi ya hekari 170,176.96.

Ameongeza kuwa TISEZA imetambuliwa kimataifa kwa kupata tuzo ya taasisi bora ya kuvutia uwekezaji barani Afrika, huku Tanzania ikiingia katika orodha ya nchi kumi bora za uwekezaji Afrika kwa mwaka 2025.

Akihitimisha hotuba yake, Prof. Mkumbo amewataka Watanzania kuendelea kulinda na kuboresha mazingira ya uwekezaji, akisisitiza kuwa uwekezaji ni msingi wa ajira, uzalishaji, teknolojia, mapato ya Serikali na ustawi wa Taifa.
Kwa Upande wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abbakari Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani utaendelea kuwa na uhakika wa gesi kupitia ujenzi wa bomba la gesi, pamoja na upatikanaji wa maji kupitia miradi ya mabwawa ikiwemo Kidunda inayotarajiwa kukamilika Desemba.

Kuhusu miundombinu, Kunenge amesema Bagamoyo ina barabara zinazopitika, reli ya TAZARA inapita mkoani humo, pamoja na uwepo wa bandari kavu itakayounganisha soko la nchi tisa za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wa viwanda, Kunenge amesema mkoa una viwanda 1,991, ambapo tangu Rais Samia aingie madarakani viwanda vipya 254 vimeanzishwa, huku vingine 27 vikitengwa.

Amesema maeneo mapya ya uwekezaji yameandaliwa, baadhi yakiwa tayari yameanza kujengwa, na yanatarajiwa kuzalisha ajira zisizopungua 10,000.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Mkoa wa Pwani ni wa kimkakati, unaosimamiwa kwa vitendo, ukiweka mkazo katika kupata mapato kupitia uwekezaji juu ya ardhi na si ardhi yenyewe.

Akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Kaimu Mkurugenzi wa  Maeneo Maalumu Kiuchumi, Anna Lyimo, amesema kuwa Mamlaka hiyo imekabidhi haki za uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo, ambayo ni hatua inayolenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uhamasishaji wa uwekezaji wenye tija.

Ameeleza kuwa uwepo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kukuza maeneo maalum ya kiuchumi na kuwezesha wananchi, hususan vijana, kupata ajira na fursa za kujiajiri.

Amesema kuwa makabidhiano ya haki kwa wawekezaji na uwasilishaji wa taarifa ya hali ya uwekezaji ni ushahidi wa utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali kwa vitendo, huku akiwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kuwekeza Bagamoyo na maeneo mengine maalum ya kiuchumi nchini.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (MB.), Akikabidhi hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, leo Desemba 30, 2025 Mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (MB.), akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, leo Desemba 30, 2025 Mkoani Pwani.
Mbunge wa Bagamoyo Subira Mgalu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, leo Desemba 30, 2025 Mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (TISEZA) Gilead Teri akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo Eco–Maritime City (BEMC) SEZ, leo Desemba 30, 2025 Mkoani Pwani.



Picha ya Pamoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...