Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAD) kwa kupandisha bendera ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) katika hafla iliyofanyika Makao Makuu yake, Banana–Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Mhandisi Furaha Sanga, amesema ICAD ni siku muhimu inayotambua mchango wa sekta ya anga katika maendeleo ya dunia, ikiwemo uchumi, biashara, utalii, mawasiliano na usalama.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu: “Safe Skies & Sustainable Future for All” ikimaanisha “Anga Salama na Mustakabali Endelevu kwa Wote.”
Mhandisi Sanga amesema kauli mbiu hiyo inaendelea kuikumbusha sekta ya anga umuhimu wa kuimarisha usalama huku ikihakikisha ukuaji endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kama sehemu ya maadhimisho ya ICAD, TCAA imetoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Elimu hiyo imejikita katika masuala mbalimbali ikiwemo majukumu ya TCAA kama mdhibiti wa sekta ya anga, usalama na matumizi sahihi ya ndege nyuki (droni), haki za abiria wa usafiri wa anga pamoja na fursa zilizopo katika taaluma za anga sambamba na kutangaza huduma zinazotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC).
Mhandisi Sanga amesema kutoa elimu kwa jamii ni hatua muhimu katika kukuza uelewa na ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya anga.
Mbali na hafla ya makao makuu, vituo vyote 15 vya TCAA nchini vimeadhimisha ICAD kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo utoaji elimu, majadiliano na wadau wa anga na mapendekezo ya maboresho ya huduma kulingana na maeneo yao.
Mhandisi Sanga amevipongeza vituo hivyo kwa ubunifu na ushiriki mkubwa, akisisitiza kuwa maadhimisho ya ICAD ni ya kitaifa na yanawahusu watumishi wote wa Mamlaka.
Ameshukuru wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya ndege, taasisi za serikali, marubani, wahandisi na washirika wa usalama wa anga kwa kuendelea kushirikiana na TCAA katika kuhakikisha anga la Tanzania linabaki salama na lenye ufanisi.
Kwa upande wa watumishi wa TCAA, Mhandisi Sanga ametoa wito wa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu, sambamba na kukumbatia mabadiliko ya kiteknolojia ili kuendana na mahitaji ya sekta ya anga duniani.
Amesema TCAA itaendelea kuboresha mifumo, huduma na usimamizi wa sekta kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ikilenga kuimarisha viashiria vya usalama kama USOAP na SASO kutoka ICAO.
Amehitimisha kwa kuwatakia watumishi na wadau wote maadhimisho mema ya ICAD 2025, akisisitiza dhamira ya Mamlaka kuendeleza kauli mbiu ya mwaka huu: “Anga Salama na Mustakabali Endelevu kwa Wote.”
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Mhandisi Furaha Sanga akipandisha Bendera ya Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Mhandisi Furaha Sanga akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD) yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Banana-Ukonga jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi wa TCAA wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Mhandisi Furaha Sanga wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani yaani International Civil Aviation Day (ICAD) yaliyofanyika Makao makuu ya Mamlaka hiyo Ukonga- Banana jijini Dar es Salaam.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...