NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

TAASISI ya HakiElimu Tanzania inaendelea na juhudi mahsusi za kushirikisha wadau wa elimu nchini ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa mtoto wa kike, hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaokatisha masomo kutokana na vikwazo vya kijinsia.

Hatua hiyo imebainishwa wakati wa warsha ya wadau wa elimu uliyohusisha Maafisa Elimu, Maafisa Mipango, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii na Marafiki wa Elimu kutoka halmashauri nane za mikoa nane ya Tanzania Bara zinazotekeleza Mradi wa Mageuzi ya Usawa ya Kijinsia katika Elimu (MMUKE).

Halmashauri hizo ni Babati Mji, Mpwapwa, Korogwe, Muleba, Kilosa, MusomaManispaa, Iramba pamoja na Mkuranga.

Akizungumza katika warsha hiyo Desemba 18, 2025 mkoani Dodoma, Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia na Maendeleo kutoka HakiElimu, Bi. Nuria Mshare, amesema taasisi hiyo inatekeleza mradi wa mageuzi ya elimu unaolenga kumuwezesha mtoto wa kike kupata elimu bila vikwazo.

Amesema mradi huo unajikita katika uboreshaji wa miundombinu rafiki kwa watoto wa kike ikiwemo ujenzi wa mabweni, vyoo vinavyokidhi mahitaji ya usafi wa hedhi, pamoja na madarasa salama ya kujifunzia.

“Tuliona umuhimu wa kukutana na wadau hawa ili kujadili changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi, na kwa pamoja tuweze kupata suluhisho zitakazowezesha kufikia malengo tuliyokusudia,” amesema Bi. Mshare.

Mradi huo, unaoratibiwa na HakiElimu kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa elimu, unalenga kujumuisha masuala ya kijinsia katika mifumo ya elimu ili kuhakikisha usawa wa fursa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Kwa upande wake, Mratibu wa Vilabu vya Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mashuleni, Bi. Imaculata Masiku Amos, ameishukuru HakiElimu kwa kuendesha mradi huo, akisema unatarajiwa kuongeza mshikamano wa viongozi na wadau katika kushughulikia vikwazo vinavyomkabili mtoto wa kike kielimu.

Naye Afisa Elimu wa Wilaya ya Babati Mji, Bw. Simon Mumbee, amesema mkutano huo umewapatia uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuingiza viashiria vya kijinsia katika bajeti za sekta ya elimu.

“Tumebaini kuwa wasichana wengi hukosa masomo wakati wa hedhi kwa sababu ya ukosefu wa taulo za kike, hivyo tumeona ni muhimu suala hili liwekwe rasmi kwenye bajeti zetu za halmashauri,” amesema Mumbee.

Ameongeza kuwa changamoto ya chakula shuleni pia imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi, jambo lililowasukuma kushirikisha wadau wilayani mwao ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wakiwa shuleni.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Regina Samson Masyole, amesema amejifunza umuhimu wa kuandaa miundombinu inayozingatia mlengo wa kijinsia, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza utoro na kuongeza ufaulu kwa wasichana

Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Bw. Mustapha Ngwila, amesema HakiElimu imeonesha maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na changamoto zake zilizojitokeza kwa mwaka 2025, huku suluhisho zikitafutwa ili kuufanikisha mradi kwa awamu ya pili.

Amesema licha ya changamoto zinazosababishwa na mila, desturi na uelewa mdogo wa jamii kuhusu masuala ya kijinsia, jamii inapaswa kutegemea matokeo chanya yatakayowezesha mtoto wa kike kupata haki yake ya elimu.

Mradi wa Mageuzi ya Usawa ya Kijinsia katika Elimu (MMUKE) unatarajiwa kufikia kilele chake mwaka 2028, huku ukitarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika elimu na kumuwezesha mtoto wa kike kusoma bila vikwazo na kufikia ndoto zake.
































Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...