Na MWANDISHI WETU, Bagamoyo
WAHITIMU wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), wamehimizwa kuilinda amani nchini.
Akizungumza katika Mahafali ya 36 ya TaSUBa, mjini Bagamoyo leo Desemba 19, 2025, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma alisema wahitimu hao kwa kiasi kikubwa ni vijana, hivyo wana wajibu wa kuitunza amani ya Tanzania kwani ni tunu.
Alisema, amani iliyopo nchini siyo jambo la kawaida bali ni tunu ya kipekee inayopaswa kulindwa na kuenziwa kila wakati.
Alisema Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa miongo mingi kutokana na busara za viongozi na mshikamano wa wananchi, hivyo ni hazina ambayo inapaswa kulindwa kwa vitendo.
“Ninapenda kutumia fursa hii kuwakumbusha wahitimu ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana kwamba, amani tuliyonayo nchini mwetu siyo jambo la kawaida bali ni tunu ya kipekee inayopaswa kulindwa na kuenziwa kila wakati.
“Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa miongo mingi kutokana na busara za viongozi na wananchi kwa ujumla, hii ni hazina ambayo mnapaswa kuilinda kwa vitendo, maneno na matendo yenu,” alisema Mwinjuma.
Alisisitiza kwamba vijana wasanii wana nafasi kubwa katika kuilinda amani na kuimarisha amani kupitia kazi zao za sanaa iwe ngoma, muziki, filamu, maigizo, uchoraji au sanaa za fasihi.
“Sanaa yenu inaweza kuwa chombo cha kuelimisha jamii, kupunguza migogoro, kujenga maelewano na kuhimiza uzalendo.
“Epukeni kutumia sanaa au majukwaa ya mitandao ya kijamii kuchochea chuki, mgawanyiko au vurugu, badala yake tumieni vipaji vyenu kuhubiri amani, umoja na mshikamano,” alisema.
Aliongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutambua mchango mkubwa wa sanaa na utamaduni wa Tanzania kwani kupitia wizara yake ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeweka sera ya kusimamia utamaduni kwa ujumla na sanaa ikiwemo ndani yake.
Kwa upande wa Mkuu wa TaSUBa, Dk. Herbert Makoye alisema wanamshukuru Rais Dk. Samia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na viongozi mbalimbali kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika taasisi hiyo.
Alisema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia ilishatoa fedha ambazo zimewasaidia kukarabati baadhi ya majengo na kununua vifaa mbalimbali vinavyotumika kufundishia na kujifunzia.
Alisema pia wamekuwa wakipata changamoto ya kukabiliwa na uhaba wa madarasa na mabweni kwani wanafunzi wamekuwa wakiongezeka kila mwaka.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia, fedha alizotupatia tumefanikiwa kukarabati baadhi ya majengo, lakini tunakabiliwa na changamoto ya madarasa na mabweni kutokana na idadi ya wanachuo kuongezeka kila mwaka,” alisema Makoye.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 234 wamehitimu ambapo 107 walimaliza astashahada na 127 wakihitu stashahada.






















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...