-Kamati ya Bunge yaiahidi ALAF ushirikiano
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imefanya ziara katika kiwanda cha ALAF limited na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na ushauri kwa bunge na serikali ili sekta ya chuma hususan kiwanda hiki kiendelee kuwa bora zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Deo Mwanyika ambaye kwa niaba ya kamati aliipongeza ALAF kwa uwekezaji mkubwa inayoendelea kufanya ili kuongeza uzalishaji.
Ametoa mfano wa mtambo wa mabati ya rangi ambao ulianza uzalishaji wake mwisho wa mwaka 2024 na kuhakikisha mabati ya rangi yanapatikana nchini tofauti na hapo awali mbapo taifa lililazimika kuagiza mabati haya kutoka nje.
“Kama kamati tulishuhudia tangu mradi huu unaanza hadi ukamilishaji wake na tunaupongeza uongozi wa ALAF kwa kuhakikisha hili linafanyika kwa wakati na tumefarajika sana kusikia kuwa mtambo huu unaendeshwa kwa asilimia 100 na vijana wa kitanzania kutoka vyuo mbalimbali ambao walipewa mafunzo na ALAF,” amesema.
Ameongeza , “Pamoja na haya mafanikio tunajua kuna changamoto mbalimbali ambazo haziwezi kukosekana ndio maana tumekuja ili tuchukue maoni yenu tukayafanyie kazi ikiwemo kuwasilisha bungeni na serekalini kwa utekelezaji.”
Ametoa mwito kwa watanzania kutumia bidhaa za ndani na kuepukana na bidhaa feki ambazo hazikidhi viwango. “Tunataka watanzania waweze kupata biadhaa zenye ubora kwa maana hiyo hatuna budi kuhakikisha vikwazo vilivyopo kwa sasa vinaondoka ili muweze kufanya biashara kwa ufanisi.”
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Bw. Bibhu Nanda ameishukuru Kamati hiyo kwa kutenga muda wa kutembelea ALAF na kusikiliza changamoto zao kama kiwanda pamoja na kujionea mafanikio yaliyopatikamna hadi sasa.
“Ikiwa tunatimiza miaka 65 tangu kiwand chetu kuanza kazi tunajivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi yetu hususan katika sekta za ujenzi, miundombinu na kilimo. Tunaendelea kuwahakikishia ubora wa hali ya juu katika uzalishaji wetu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa sababu tunaelewa wajibu wetu kwa jamii,” alisema.
Awali Meneja Uhusiano na Mawasiano wa ALAF, Hawa Bayumi ametoa rai kwa Watanzania wapende vya nyumbani na kusisitiza kuwa kwa msaada wa kamati hii ya bunge, wanaamini serikali itatatua changamoto zote ambazo zinaathiri uzalishaji kwa sasa.
“Tukiwa tunaishukuru serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, tunaiomba indelee kutatua changamoto zilizopo ili tupate ufanisi na kufungua fursa zaidi hususan kwa vijana,” amesema.
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza suluisho za ujenzi. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...