Na Mwandishi wetu, Simanjiro


WILAYA ya Simanjiro mkoani Manyara, imejipanga kuhakikisha inafanya mageuzi makubwa katika mazao ya kilimo na mifugo ili wakazi wa eneo hilo wapate tija zaidi na kunufaika kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mwalimu Fakii Raphael Lulandala ameeleza hayo kwenye kongamano la kilimo la mwaka 2025/2026 lililofanyika mji mdogo wa Orkesumet

Lulandala amesema Simanjiro ina maeneo makubwa ya kilimo na yenye rutuba ikiwemo ya umwagiliaji ila bado hayajatumika ipasavyo katika kulima, hivyo wahitaji wachangamkie fursa hiyo.

"Simanjiro imetenga kiasi cha hekta 17,000 kwa ajili ya kilimo ila hadi sasa zinatumia hekta 630 pekee kwa kulima, tunawakaribisha wakulima waje Simanjiro kwani tumejipanga kisawasawa maeneo ya kilimo yapo," amesema DC Lulandala.

Mkuu huyo wa wilaya ametaja baadhi ya mazao yanayostawi kwenye eneo hilo ni pamoja na mahindi, maharage, vitunguu, mpunga na ufuta.

Hata hivyo, amewaagiza maofisa ugani kuhakikisha wanahamia mashambani kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima na kutobakia maofisini kwao.

"Maofisa ugani ofisi zenu ziwe mashambani badala ya ofisini kwani waajiri wenu huwa wanapatikana mashambani hivyo tusikae maofisini kwetu," amesema DC Lulandala.

Mmoja kati ya wakulima katika wilaya hiyo Ibrahim Abdalah ameeleza kwamba kongamano hilo limekuwa na manufaa kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo za kilimo kwa wakati tofauti na awali.

Abdalah amesema awali walinyanyasika mno kwa mbegu feki na wakulima kutopata mbegu zenye ubora hivyo kupata wakati mgumu kuvuna mazao ya maana ila kupitia kongamano hilo la mazao ya kilimo mbegu nyingi zenye ubora zimewafikia.

Bwana shamba mauzo wa kampuni ya mbegu ya Seedco Peter Timotheo ameeleza kwamba wamewajali wakulima wa Simanjiro kwa kuwapatia mbegu bora kwani mavuno bora huanza na mbegu bora.

Timotheo amewaasa wakulima wa wilaya ya Simanjiro kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kuwepo kwa mbegu zao bora na kuzichukua ili wapate mavuno bora.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...