Na Khadija Kalilli,Kibaha
KAIMU Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Kibaha na Chalinze kuimarisha usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma, ikiwemo mapato na fedha za Serikali, pamoja na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha ili kuongeza tija na manufaa kwa wananchi.
Akizungumza leo Januari 16, 2026, wakati wa kuhitimisha mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo madiwani hao, Twamala amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha madiwani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, ili kuleta matokeo chanya yanayoonekana moja kwa moja kwa wananchi. Alisisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona mabadiliko ya kweli yatokanayo na maarifa na ujuzi walioupata kupitia mafunzo hayo.
Ameeleza kuwa madiwani wanapaswa kuzingatia misingi ya utawala bora, kuheshimu sheria, kanuni na taratibu, pamoja na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, hususan katika kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta mbalimbali.
Aidha, amewataka madiwani hao kutafsiri kwa vitendo vipaumbele vya Serikali kupitia utekelezaji wenye tija wa majukumu yao, huku wakizingatia maslahi mapana ya wananchi wanaowawakilisha.
Katika hatua nyingine, Twamala amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na wananchi, sambamba na kuepuka migogoro isiyo ya lazima inayoweza kukwamisha maendeleo. Ameongeza kuwa madiwani wanapaswa kuzingatia utu, utulivu, kujitawala kihisia na kusikiliza kwa makini kero na changamoto za wananchi ili kuzitatua kwa busara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Mhe. Hasani Mwinyikondo, Diwani wa Kata ya Msoga, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa madiwani katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo, fedha za umma na masuala ya utawala bora.
Mhe. Mwinyikondo amebainisha kuwa mada zilizotolewa ni pamoja na uongozi na utawala bora, sheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli za Serikali za Mitaa, uendeshaji wa vikao, uandaaji wa mipango na bajeti, usimamizi na udhibiti wa fedha, usimamizi wa rasilimali watu, haki na stahiki za viongozi, pamoja na maadili ya uongozi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utendaji wa madiwani na kuongeza ufanisi katika kusimamia maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Kibaha na Chalinze.


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...