Na Pamela Mollel,Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kusogeza huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo karibu na wananchi.
Anasema uanzishwaji wa Kituo cha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Centre (Seliani) utawanufaisha wananchi wa Arusha na mikoa ya jirani, pamoja na watalii na wageni watakaoshiriki michuano ya AFCON 2027.
Mhe Makalla anayasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua zoezi la utoaji wa vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bure, ambapo jumla ya wananchi takribani 1,200 wamenufaika na huduma hizo, huku Serikali ikiahidi kuwawezesha wananchi wasiokuwa na uwezo wanaohitaji rufaa ili wapate matibabu zaidi katika Taasisi ya Moyo ya JKCI jijini Dar es Salaam.
Aidha, amewahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amesema katika Kanda ya Kaskazini, magonjwa ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuonekana kwa kasi, ambapo kupitia programu ya upimaji wa afya, zaidi ya wananchi 3,000 wamejitokeza kupima afya zao.
Anasema kuwa kati yao, asilimia 9 walibainika kuwa na matatizo ya moyo, huku asilimia 29 wakigundulika kuwa na shinikizo la damu, ugonjwa uliokuwa unaongoza zaidi kwa wananchi wenye umri kati ya miaka 45 hadi 80
Dkt. Kisenge ameongeza kuwa sababu kuu zinazosababisha ongezeko la magonjwa hayo ni kutofanya mazoezi ya mwili, unene uliopitiliza, unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, pamoja na kutokuzingatia lishe bora, akiwahimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuepuka madhara makubwa ya kiafya.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...