Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Jamhuri ya Malawi  Madalitso Baloyi, amesema serikali ya nchi yake inaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wake kwa kushirikiana na Tanzania, kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Baloyi ameyasema hayo leo Januari 16, alipotembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, amesema wamefika kujifunza masuala ya afya, akibainisha kuwa Tanzania imekuwa kinara katika utoaji wa huduma za afya. 

Amesema mwaka 2025 Malawi ilipokea timu ya wataalamu kutoka hospitali hiyo, jambo lililowapa uzoefu na kuwahamasisha kuendeleza ushirikiano huo.

Amesema kwa sasa wagonjwa wengi kutoka Malawi hulazimika kupelekwa katika nchi mbalimbali kwa ajili ya matibabu, ikiwemo India, hali inayosababisha gharama kubwa kutokana na umbali na gharama za matibabu, kwa msingi huo, Malawi inaona fursa ya kushirikiana na Tanzania ili wagonjwa wake wapate huduma za matibabu karibu na nyumbani na hivyo kupunguza gharama.

Katika ziara hiyo, Baloyi ametembelea hospitali na kukutana na baadhi ya wataalamu wa kada ya afya kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujionea ubora wa huduma zinazotolewa, amesema wamefaidika kwa kiasi kikubwa na ziara hiyo na kwamba wanaendelea kuhamasisha ushirikiano wa Kusini kwa Kusini na ndani ya Jumuiya ya SADC, pamoja na kuongeza ushirikiano katika ugavi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof. Abel Makubi, amesema hospitali hiyo imejipanga kushirikiana na nchi yoyote kimatibabu, ameongeza kuwa hospitali imejipanga kuzijengea uwezo hospitali mbalimbali nchini Malawi, kwa lengo la kubadilishana uzoefu.

Amesema watajikita pia katika utalii wa kimatibabu, unaosaidia kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu ya uhakika pamoja na kuongeza uzoefu wa kitaalamu.

Prof. Makubi amefafanua kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ina huduma za kibingwa ikiwemo upandikizaji wa figo, uloto, pamoja na upasuaji wa moyo, ubongo, mifupa na huduma nyinginezo, zinazovutia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali. 

Amesema hospitali imefungua njia ya kushirikiana na nchi zote za SADC na nyinginezo, kwa sababu huduma zimeboreshwa kwa kiwango cha juu, na wagonjwa wanaweza kutibiwa bila ulazima wa kwenda mataifa ya Ulaya, ambapo pande zote zinanufaika na ushirikiano huo.

Ziara hiyo inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya Malawi na Tanzania, huku ikiweka msingi wa matibabu na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa pande zote.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...