Katibu wa Uenezi, Itikadi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, anatarajiwa kuanza ziara yake ya kimkakati nchi nzima itakayozinduliwa rasmi Januari 18, 2026 Wilayani Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 17 jijini Dodoma, amesema ziara hiyo itahusisha kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Singida na kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

Amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini ili kutatua changamoto zao, kuisimamia serikali, kuimarisha uimara wa chama, pamoja na kuhakikisha maendeleo ya wananchi kwa kufuatilia utekelezaji wa ahadi za Rais alizozitoa kipindi cha kampeni, ikiwemo ahadi ya kutekelezwa ndani ya siku 100, ili kubaini utekelezaji wake umefikia wapi au matarajio ya lini zitatimia.

Ameeleza kuwa katika ziara hiyo ya nchi nzima, CCM itahakikisha inawakumbusha wananchi wapi nchi ilipotoka na ilipo sasa, akitolea mfano maendeleo katika sekta ya umeme ambapo kwa sasa vijiji vyote nchini vimefikiwa na huduma ya umeme, na sasa ni zamu ya vitongoji vyote kupata huduma hiyo.

Akigusia wajibu wa chama, amesema ni kusikiliza wananchi na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi, akisisitiza kuwa watu wote ni sawa na hakuna aliye muhimu kuliko mwingine. Amesema ni jukumu la jamii kuangalia vyama vyenye ajenda ya umoja, mshikamano na amani.

Ameongeza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itafanya kazi kwa karibu sana na wananchi, ambapo ziara hiyo itafika hadi ngazi za mashina, matawi na kata, pamoja na kukutana na mabalozi wa CCM ambao ni msingi imara wa chama katika kuwafikia wananchi wote kwenye maeneo yao.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wote wa umma wanaotambua kuwa kuna kero zitakazotolewa na wananchi zitakazowagusa moja kwa moja, kuhakikisha wanahudhuria mikutano yote ya ziara hiyo kwa ajili ya kutoa majibu na ufumbuzi wa changamoto hizo..



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...