Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeagizwa kuongeza juhudi za udhibiti wa sekta ya fedha kwa lengo la kuwalinda wananchi dhidi ya athari za kukopa katika taasisi zisizo rasmi, hali inayosababisha wengi wao kupoteza mali na rasilimali zao za thamani kutokana na mikopo yenye masharti kandamizi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB), kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika tarehe 21 Januari 2026 katika Viwanja vya Usagara mkoani Tanga.

Katika hotuba hiyo, Waziri wa Fedha amebainisha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakipata athari mbalimbali kutokana na kukopa fedha katika taasisi zisizo rasmi, hivyo kusisitiza umuhimu wa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu uhalali wa taasisi za kifedha kabla ya kukopa.

Amehimiza wananchi kusoma na kujiridhisha na mikataba ya mikopo wanayoingia ili kuepuka hasara zinazotokana na kusaini mikataba bila kuelewa masharti yake.

Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Bw. Kennedy Komba, amesema kuwa katika kutekeleza sera za ujumuishi wa kifedha na kuongeza uwazi, ulinzi na ufikikaji wa huduma kwa watumiaji wa huduma za fedha, hususan kwa wale wenye malalamiko dhidi ya watoa huduma au wanaokosa taarifa kamili kuhusu gharama, tozo na utaratibu wa ukokotoaji wa riba na mikopo, BoT imeanzisha na kuimarisha mifumo mbalimbali.

Mifumo hiyo ni pamoja na mifumo ya uwasilishaji na usimamizi wa malalamiko (SEMA na BOT), kilinganishi cha bei, kikokotoo cha gharama za mikopo, pamoja na utaratibu wa usimamizi shirikishi kwa watoa huduma ndogo za fedha wa kundi la pili, hatua ambazo zimeongeza uwazi, ufanisi na ubora wa huduma za fedha zinazotolewa kwa wananchi kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizopo.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 26 Januari 2026, yanalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya fedha na matumizi ya huduma rasmi za fedha kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...