Na Mwandishi Wetu, WMTH-Dar es Salaam


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kifedha na kitaasisi ili kuchochea uvumbuzi unaojenga ajira na kujitegemea kwa Taifa.

Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo Januari 19, 2026, akifungua Kongamano la 9 la Mwaka la TEHAMA (TAIC 2026), jijini Dar es Salaam. Na kuelezea furaha yake kuona jukwaa hili likitenga siku ya hii kwa ajili ya wanawake katika TEHAMA. Huku akisema kuwa hatua hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Wanawake na Wasichana wanashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kidijitali na uvumbuzi wa kiteknolojia.

“Wanawake wana mchango mkubwa katika kuendeleza TEHAMA, kuanzisha bunifu, kuongoza taasisi za kidijitali, na kubuni suluhisho zenye athari chanya za kijamii,” alisisitiza Mhe. Kairuki.

Waziri Kairuki pia alisisitiza umuhimu wa vijana katika mabadiliko ya kidijitali, huku akieleza kuwa kupitia kampuni changa za TEHAMA (ICT Startups), vijana wetu wana fursa kubwa ya kujiajiri badala ya kuajiriwa.

“Ni malengo ya Serikali kuwa kundi hili litambulike, liendelezwe na liungwe mkono kwenye kuboresha ubunifu wao,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alieleza hatua za kimkakati zinazochukuliwa na Serikali ili kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanatekelezwa kwa ufanisi. Aliiagiza Tume ya TEHAMA kuimarisha usajili na uendelezaji wa wataalam wa TEHAMA pamoja na kuimarisha mifumo ya kusimamia na kusaidia kampuni changa bunifu za TEHAMA ili bidhaa na huduma zao ziweze kuingia sokoni kwa ufanisi. Aidha, alizitaka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuhakikisha zinawasilisha taarifa kuhusu mifumo yao ya TEHAMA kwa Wizara, na kuhakikisha mifumo hiyo inavyosomana na mifumo mingine.

Waziri Kairuki alisisitiza pia umuhimu wa wabunifu na waandaaji wa maudhui (“Content Creators”) kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya mifumo na teknolojia zinazoibukia, kama vile Akili Unde (AI), ili kuepuka matumizi yanayokiuka maadili ya nchini.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...