Farida Mangube, Morogoro 

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) leo Januari 27, 2026 imeshiriki Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti #27Yakijani kwa kupanda miti ya asili aina ya Mkongo (Afzelia quanzensis), kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa mazingira na kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Zoezi hilo liliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, kwa kushirikiana na Watumishi wa Taasisi hiyo kutoka Makao Makuu na Vituo vya Utafiti, na kufanyika katika moja ya maeneo ya shamba la miti la Taasisi. 

Akizungumza na Waandishi wa habari, Dkt. Mushumbusi alisema upandaji wa miti ya Mkongo unalenga kurejesha miti ya asili yenye thamani kubwa na iliyo hatarini kutoweka, sambamba na kuimarisha uhifadhi wake.

Aliongeza kuwa ushiriki wa TAFORI katika kampeni hiyo ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kitaasisi wa kufanya utafiti, kuratibu na kusambaza matokeo ya utafiti wa misitu na ufugaji nyuki, kwa lengo kuu la kuendeleza uhifadhi miti ya asili na mingineyo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuonesha mfano wa namna sahihi ya upandaji wa miti katika maeneo husika.

Zoezi la 27Yakijani linaongozwa na kaulimbiu “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti”, kaulimbiu inayoakisi dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza ajenda ya Taifa ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji miti, ulinzi wa vyanzo vya maji, kuimarisha uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda mti wa muembe (Mangifera indica) katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, kama Kiongozi na mdau wa mfano katika kulinda na kutunza mazingira.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...