Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi akielezea vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja na filamu ya Tanzania: The Royal Tour, wakati wa Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Matka, yanayoendelea jijini Helsinki, Finland.
UBALOZI wa Tanzania nchini Sweden umeratibu na kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Matka yanayofanyika jijini Helsinki, Finland, kuanzia tarehe 14-18 Januari, 2026, huku ukitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja na filamu ya Tanzania: The Royal Tour.
Maonesho hayo ni miongoni mwa maonesho makubwa barani Ulaya yakijumuisha kampuni 950 za utalii, usafiri wa ndege, vyombo vya habari, na ushauri elekezi wa utalii kutoka duniani kote ambapo katika siku ya kwanza yalipokea washiriki 56,000 wakiwemo watalii watarajiwa.
Kampuni binafsi za Lifestyle Safaris & Holidays na Lifetime Safaris za Tanzania nazo zinashiriki katika maonesho hayo zikiwa na timu ya Ubalozi wa Tanzania. Nchi zingine za Afrika zinazoshiriki ni Uganda, Kenya, Ushelisheli, Namibia, Afrika Kusini, Senegal, Moroko, Tunisia na Misri.
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, anayeiwakilishia pia Tanzania katika nchi za Nodiki, Baltiki na Ukraina, alitumia jukwaa kuelezea namna Tanzania ilivyopata heshima kubwa ya kushinda Tuzo za Utalii za Dunia tarehe 6 Desemba 2025, nchini Bahrain, ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo.
Balozi Matinyi alielezea pia namna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyoshiriki na kuigiza katika filamu ya kuitangaza Tanzania ya dakika 57 iitwayo Tanzania: The Royal Tour akiwa na mwandishi wa Marekani mshindi wa Tuzo ya Emmy, Peter Greenberg, mwaka 2022.
Balozi Matinyi aliiambia hadhira kwamba Tanzania ina vivutio vitatu kati ya Maajabu Saba ya Asili ya Afrika na pia maeneo saba yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama Urithi wa Dunia, akiutaja mathalani Mlima Kilimanjaro, uhamaji mkubwa wa wanyamapori hifadhini Serengeti na bonde la Ngorongoro. Mbali ya hifadhi za taifa 22, Balozi Matinyi pia alitaja utajiri wa utamaduni wa makabila 126 ya Tanzania, hifadhi za historia ya kale kama michoro ya mapangoni ya Kondoa, Mji Mkongwe wa Zanzibar na miji ya Bagamoyo na Kilwa.
Balozi Matinyi pia alitumia maonesho hayo kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wakiwemo Afisa Mtendaji Mkuu wa Atlantic Link, Bi. Karin Gert Nielsen na Mwakilishi wa Danish Travel Show, zote za Denmark, Bw. Johnny Frandsen; Meneja wa kampuni ya Flygresor ya Sweden, Bw. Peter Hallgren; na kwa kampuni za Finland Mwanzilishi na Mkurugenzi Mwendeshaji wa GapEdu, Bw. Jyrki Nilson; Mkurugenzi Mwendeshaji wa Amanihoiva Limited, Bw. Juha Valtanen na Mwakilishi wa Matka Travel Fair, Inkeri Vainik. Mazungumzo hayo yalilenga namna ya kushirikiana katika kuutangaza zaidi utalii wa Tanzania barani Ulaya.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Tanzani nchini Sweden,
17 Januari, 2025.
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, akizungumza na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya GapEdu ya Finland, Bw. Jyrki Nilson, kwenye banda la Tanzania wakati wa Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Matka, yanayoendelea jijini Helsinki, Finland.
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi (kulia) pamoja na Afisa Ubalozi Abel Maganya, wakizungumza na Bw. Peter Hallgren wa kampuni ya Flygresor ya Sweden kwenye banda la Tanzania wakati wa Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Matka, yanayoendelea jijini Helsinki, Finland.




.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...