Na Pamela Mollel,Arusha

Wawekezaji wazawa wadogo na wa kati wamepata fursa adhimu ya kuunganishwa moja kwa moja na vyanzo vya mitaji, masoko pamoja na vivutio mbalimbali vya uwekezaji, kupitia jukwaa maalum lililoandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) pamoja na Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC).

Jukwaa hilo, lililofanyika mkoani Arusha, liliwakutanisha wawekezaji wa ndani kwa lengo la kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuwaunganisha na taasisi za kifedha, pamoja na kuwapatia mwongozo wa namna ya kupata mitaji kwa ajili ya kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa na huduma za ndani.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gerald Teri, aliwahimiza wawekezaji wazawa kusajili miradi yao ili kupata Vyeti vya Uwekezaji, akieleza kuwa vyeti hivyo vinatoa ulinzi wa kisheria pamoja na vivutio mbalimbali ikiwemo msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa forodha kwa mashine na vifaa vya uzalishaji.

Kwa upande wa upatikanaji wa mitaji, Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) ilieleza dhamira yake ya kusaidia wawekezaji wadogo na wa kati kupitia mikopo yenye masharti nafuu, hususan kwa miradi ya viwanda na biashara zinazoongeza thamani.

Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkurugenzi wa Mipango wa TIB, Joseph Felix Chilambo, alisema benki hiyo inalenga kuhakikisha changamoto ya mtaji haiwi kikwazo kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.

Naye Rais wa TNCC, Vicent Minja, alisisitiza kuwa jukumu kuu la chemba hiyo ni kuwaunganisha wawekezaji wazawa na masoko ya ndani na ya kimataifa. Alibainisha kuwa kupitia mtandao mpana wa TNCC, mwekezaji mdogo kutoka Arusha anaweza kupata washirika wa kibiashara kutoka sehemu mbalimbali duniani, hali itakayochochea uhamishaji wa teknolojia, kuongeza ufanisi na kuimarisha ushindani katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa EABC, Iman Kajula, alisema jukwaa hilo ni muhimu kwa wawekezaji wengi wa Kitanzania, hususan wale wanaokabiliwa na changamoto ya kutambua na kufikia fursa mpya za uwekezaji. Aliongeza kuwa mkutano huo umefungua milango kwa wafanyabiashara kujifunza, kuunganishwa na wadau sahihi, pamoja na kuchukua hatua za vitendo kuanzisha au kupanua uwekezaji wao.

Jukwaa hilo lilidhaminiwa na Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), likiwa ni sehemu ya jitihada za pamoja za kukuza uwekezaji wa wazawa na maendeleo ya uchumi wa Taifa.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...