Na Mwandishi Wetu,Kilimanjaro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 25 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa Kikao cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi kilichofanyika mwaka 2024 lengo ikiwa kuifanyia maboresho Shule cha Polisi Kilimanjaro ambacho kinakabiliwa na uchakavu wa Majengo ambayo yalijengwa tangu mwaka 1933 ambapo yanajumuisha Mabweni ya Wanafunzi,Madarasa na Nyumba za Askari.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama(NUU) iliyotembelea shule hiyo kukagua matumizi ya fedha hiyo iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ikiwa ni utaratibu wa Kamati za Bunge kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Leo tunazungumza Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo Rais ameweza kuyafanya haya ambayo wajumbe mmeyashuhudia leo kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 25 ambazo mmeona kwa kiwango kikubwa na uweledi mkubwa wa jeshi katika utekelezaji na uwezo wa kusimamia kazi.Kwa kweli hatuna namna ya kuweza kumshukuru Mheshimiwa Rais Zaidi ya kumuombea afya njema,umri na rizki ili Mwenyenzi Mungu aendelee kumpa hekima na busara ili sisi wizara tuendelee kuwa wanufaika wa uongozi wake” amesema Waziri Katambi
“Lakini tuna miradi ya ujenzi wa nyumba sehemu mbalimbali ambapo Mheshimiwa Rais pia anatoa kiasi kikubwa cha fedha na pale Dodoma tayari mradi ushaanza na tunatumia wataalamu wetu wa ndani na wanajenga kwa viwango vile vile kama mlivyoona hapa Shule ya Polisi,tunaenda kufanya maboresho ya maslahi kwa askari,mabadiliko ya sera na sheria na teknolojia za kisasa pia zinaendelea kuingizwa jeshini ili vifaa vya kisasa vitumike katika kulinda usalama wetu.”Aliongeza Waziri Katambi
Akizungumza katika ziara hiyo,Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya NUU, Najma Murtaza Giga, ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa kujenga mradi huo kwa ufanisi na uweledi mkubwa huku akikiri kuona thamani ya kiasi cha fedha kilichotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan huku akiweka wazi Kamati kuendelea kuwa na imani na Jeshi la Polisi katika masuala mbalimbali na hivyo haina budi kuendelea kulisemea Jeshi la Polisi kuhakikisha linawezeshwa ili liweze kutekeleza majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.
Nae Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, ameishukuru Kamati hiyo ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa kutenga muda na kuona umuhimu wa kutembelea Shule ya Polisi Tanzania-Moshi mkoani Kilimanjaro na kuona thamani ya fedha iliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyotumika kwa kuhakikisha ubora na ufanisi unaonekana kwenye miradi hiyo ya ujenzi.
Aidha, IGP Wambura, ameiambia kamati hiyo kuwa, serikali ya awamu ya sita imeendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kwenye miundombinu mbalimbali kote nchini ili kuhakikisha askari Polisi wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri na wezeshi katika kuwahudumia wananchi, kutatua kero mbalimbali ili waendelee kufanya kazi zao bila uwepo wa matishio ya kihalifu nchini.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...