📌Miundombinu mipya imerahisisha usafirishaji wa vikonyo vya mimea na kuchochea maendeleo Arumeru

Arumeru, Arusha

Wananchi wa kijiji cha Duluti wilayani Arumeru mkoani Arusha wameweka mkakati wa kupanda miti kandokando ya barabara mpya ya lami ya Sangisi-Nambala yenye urefu wa Km 4.2 iliyojengwa katika eneo hilo ili kulinda miundombinu dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na kuhakikisha inadumu kwa muda mrefu.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi kunufaika na ujenzi wa barabara hiyo iliyojengwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambapo kipande cha Km. 2.36 kimekamilika 

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mwenyekiti wa kijiji cha Duluti Bw. Harisi Kaaya, amesema wananchi wameamua kuchukua jukumu la kulinda barabara hiyo kwa kupanda miti katika maeneo maalum kandokando ya barabara kwani  kwa miaka mingi ilikua katika hali mbaya na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo, wananchi walifanya kikao na mkandarasi wa mradi huo ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu umbali unaofaa wa kupanda miti bila kuathiri miundombinu ya barabara.

“Tumekaa kikao na kumuomba mkandarasi atuoneshe umbali sahihi wa kupanda miti ili kuilinda barabara hii. Sisi wananchi tuna dhamira kubwa ya kuitunza kwa sababu tumekaa miaka mingi sana bila kuwa na barabara ya lami na tumeteseka kwa muda mrefu,” amesema Kaaya.

Ameeleza kuwa tangu wakiwa watoto hawakuwahi kushuhudia barabara ya lami katika eneo hilo, kwani kwa muda mrefu barabara hiyo ilikuwa ikitumika zaidi kupitisha mazao ya kahawa pamoja na mazao mengine ya kilimo kutoka maeneo ya chini kwenda sokoni.

Ameongeza kusema kwamba wakati wa mvua barabara hiyo ilikuwa haipitiki kabisa kutokana na mmomonyoko wa ardhi na maji ya mvua yaliyokuwa yakiharibu miundombinu hiyo.

“Tunamshukuru Mungu na serikali kwa sasa kuwa na barabara ya kiwango cha lami. Zamani wakati wa masika barabara ilikuwa haipitiki kabisa kutokana na maporomoko ya mvua na uharibifu wa barabara,” amesema.

Kaaya ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umeleta nafuu kubwa kwa wananchi kwa kupunguza gharama za usafiri na kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda katika Soko la Tengeru.

“Kwa kweli tuna furaha sana. Hapo awali tulikuwa tunalipa nauli ya shilingi 2,000 kufika Tengeru, lakini kwa sasa tunalipa takribani shilingi 500 kwa kutumia bajaji. Hii imerahisisha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za biashara,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa kampuni inayojihusisha na usafirishaji wa vikonyo vya maua katika eneo hilo Bw. Nelson Shilinde, amesema ujenzi wa barabara ya lami ya Malalua-Nduruma-Bwawani Km. 28 ambapo kwasasa kipande cha mita 650 kimekamilika umekuwa na manufaa makubwa kwa shughuli zao za kilimo.

Amesema hapo awali vumbi lililotokana na ubovu wa barabara lilikuwa linaathiri mimea yao, kwani vumbi lilikuwa linaganda kwenye plastiki za ‘greenhouses’ na kuzuia mwanga wa jua kupenya ipasavyo.

“Mimea yetu inahitaji mwanga wa kutosha wa jua ili kustawi. Zamani vumbi lilikuwa linaganda kwenye plastiki  na kuathiri ukuaji wa mimea. Lakini sasa hali hiyo haipo kutokana na ujenzi wa barabara ya lami,” amesema.

Amesema pia usafirishaji wa miche na mazao yao umeboreshwa kwa kiasi kikubwa, kwani magari yao sasa yanapita kwa urahisi bila kuharibika mara kwa mara kama ilivyokuwa awali.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...