Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dr Linda Salekwa (katikati) na wageni wengine wakipiga makofi wakati Shirika la UNDP pamoja na Serikali ya Finland wakitambulisha biashara bunifu 14 ndogo ndogo na za kati (MSMES) kupitia mpango wa #GreenCatalyst.  Hafla hiyo ilifanyika Mjini Njombe.
Meneja wa Programu ya FUNGUO, Joseph Manirakiza.
Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa UNDP, John Rutere

*Wazindua awamu ya pili ya maombi ya ufadhili

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, kupitia programu yake kinara ya ubunifu ya FUNGUO inayofadhiliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), na Serikali ya Finland, zimetambulisha rasmi Biashara Ndogo, Ndogo za Kati (MSMEs) bunifu 14 chini ya mpango unaoungwa mkono na Finland unaojulikana kama #GreenCatalyst.

Hatua hii inaashiria mafanikio muhimu katika kukuza ujasiriamali endelevu na uzalishaji wa ajira ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu nchini Tanzania.

Tukio la uzinduzi, lenye kaulimbiu “Kuchochea Ubunifu na Ujasiriamali katika Mnyororo wa Thamani wa Misitu” limewakutanisha wadau kutoka Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ili kuonesha biashara zilizochaguliwa na kuangazia fursa mpya za uwekezaji katika sekta hiyo.

Kwa kuongezea, tukio hilo limetumika pia kama fursa ya kuzindua rasmi awamu ya pili ya maombi ya ufadhili wa ruzuku ya kuchochea ukuaji, ikialika kundi jipya la wabunifu wa biashara endelevu zinazozingatia mustakabali wa mazingira, kuwasilisha maombi yao.

Mpango wa #GreenCatalyst ni sehemu ya FUNGUO, programu kinara ya ubunifu chini ya UNDP inayofadhiliwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) na Serikali ya Finland. Kwa ufadhili maalum kutoka Finland, mpango huu unachochea ubunifu na ujasiriamali endelevu katika mnyororo wa thamani unaojikita kwenye misitu, huku ukihamasisha ukuaji wa ajira vijijini na kufungua fursa za uwekezaji katika Biashara Ndogo, Ndogo za Kati.

Mpango huu unakamilisha mradi wa FORLAND unaojikita katika Misitu, Matumizi ya Ardhi na Mnyororo wake wa thamani, unaofadhiliwa na Finland, ambao unachangia malengo mapana ya Tanzania ya usimamizi endelevu wa rasilimali, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na ukuaji wa uchumi shirikishi.

Katika awamu ya kwanza ya ufadhili, #GreenCatalyst iliwezesha Biashara Ndogo, Ndogo za Kati bunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu, hususani zile zinazoongozwa au kunufaisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi.

Kutokana na maombi 160 yaliyopokelewa mwaka 2025, biashara 14 zilichaguliwa kupitia mchakato makini uliopitia tathmini za hatua mbalimbali ulioongozwa na kamati huru ya uwekezaji. Biashara hizi zilipokea zaidi ya shilingi bilioni moja za Kitanzania kama ruzuku, pamoja na msaada endelevu wa kiufundi. Biashara hizi zinawakilisha wigo mpana wa ubunifu ikiwemo uchakataji wa mbao rafiki kwa mazingira, ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali, bidhaa za mianzi, mafuta kwa matumizi tofauti, pamoja na huduma za kidijitali zinazohusu misitu. Biashara hizi tayari zinaonesha uwezo mkubwa wa kutengeneza ajira, kuboresha maisha ya wananchi, na kuchangia usimamizi endelevu wa misitu katika ngazi tofauti za jamii.

Meneja wa Programu ya FUNGUO wa UNDP, Joseph Manirakiza, amesisitiza kuwa awamu ya pili ya maombi ambayo itakuwa wazi mpaka Mei 31, 2026 inalenga kusaidia Biashara Ndogo, Ndogo za Kati za Kitanzania zilizo katika hatua za awali au zinazokua ndani ya mnyororo wa thamani wa misitu kupitia ufadhili chochezi, ili kufungua fursa za biashara endelevu rafiki kwa mazingira, kuzalisha ajira na kubadilisha uchumi wa vijijini.

Aliongeza kuwa kipaumbele kimewekwa kwa biashara bunifu zinazojumuisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, na zinazofanya shughuli zake au kujumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi. Sekta zinazolengwa ni pamoja na uchakataji wa mbao, bidhaa rafiki kwa mazingira, mbadala wa mkaa, useremala na samani, ufugaji nyuki, ubunifu wa mianzi, mafuta kwa matumizi tofauti, na huduma za kidijitali za misitu.

Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa UNDP, John Rutere, alieleza dira pana ya mpango huo: "Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususani misitu. Rasilimali hizi si muhimu tu kwa mustakabali uendelevu wa mazingira bali pia zinatoa fursa kubwa za ukuaji wa uchumi, ubunifu na ajira. Changamoto kubwa inayotukabili ni kunufaika na rasilimali hizi kwa uwajibikaji ili kutengeneza ajira zenye staha, hasa kwa vijana, huku tukilinda mazingira kwa vizazi vijavyo. Hili ndilo lengo kuu la #GreenCatalyst."

Aliongeza kuwa kwa kuunganisha ubunifu na upatikanaji wa fedha, ujuzi na masoko, mpango huu unasaidia kubadilisha mawazo endelevu rafiki kwa mazingira kuwa biashara halisi zinazozalisha kipato na ajira katika jamii, na kutoa shukrani kwa Serikali ya Finland kwa ushirikiano wake endelevu.

Akithibitisha dhamira ya Finland, Mratibu - Ushirikiano wa Maendeleo, William Nambiza alisema: "Finland itaendelea kujizatiti katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa misitu endelevu nchini Tanzania. Kupitia miradi kama #GreenCatalyst, tunasaidia kufungua fursa kwa vijana na wanawake, na kuhakikisha sekta hii inachangia kikamilifu ajira, ubunifu na ukuaji wa uchumi shirikishi, husasani katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini."

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. Dkt. Linda Salekwa, alitoa pongezi kwa mradi huo na kuahidi ushirikiano wa serikali: "Tunaipongeza Serikali ya Finland na UNDP kwa mpango huu wenye manufaa kubwa. Kama serikali, tunaendelea kujenga mazingira wezeshi yatakayoruhusu biashara hizi kukua, kustawi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa ndani pamoja na uhifadhi wa mazingira, hasa katika Nyanda za Juu Kusini."

Aliongeza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona vijana na wanawake wakipewa kipaumbele kupitia ujasiriamali, makundi ambayo serikali inaendelea kuyainua kwa jitihada kubwa na kuiwezesha Tanzania kufanikisha lengo lake la kufikia uchumi wa Dola Trilioni Moja.

Biashara bunifu zinazofanya shughuli zake katika mnyororo wa thamani wa misitu katika mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma na Lindi zinahimizwa kuwasilisha maombi ya ufadhili wa ruzuku wa #GreenCatalyst kupitia tovuti ya www.Funguo.org kabla ya Mei 31, 2026.

Programu ya Ubunifu ya FUNGUO ni hatua ya kimkakati ya kuchochea na kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania kwa kuwezesha biashara au kampuni changa zinazoongozwa na vijana na Biashara Ndogo, Ndogo za Kati ubunifu, kukua na kuwa biashara endelevu na zinazovutia uwekezaji. Inatekelezwa na UNDP Tanzania kwa msaada wa Umoja wa Ulaya, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) na Serikali ya Finland. FUNGUO inalenga kuziba pengo lililopo katikati ya mfumo wa ubunifu (“missing middle”), ambapo biashara nyingi zenye uwezo zipo lakini hushindwa kupata mitaji, huduma bora za maendeleo ya biashara, na sera rafiki. Mpango huu unatekelezwa kupitia nguzo tatu kuu: Ufadhili chochezi wa ubunifu, Kuimarisha utoaji wa huduma za ubunifu, na Kuboresha mazingira wezeshi kwa biashara zinazoongozwa na vijana na wanawake.

Kupitia mbinu hii, FUNGUO hupunguza hatari za ubunifu katika hatua za awali kwa kutoa ruzuku pamoja na msaada wa kiufundi, kusaidia biashara kujijenga, kuboresha mifumo ya kiuongozi, na kuwa tayari kuvutia wawekezaji. Hili hutekelezwa kwa jitihada thabiti endelevu, ikiwemo mpango mashuhuri wa #YouthIgnite unaowawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kubadili mawazo yao kuwa biashara halisi, pamoja na kuimarisha taasisi za kusaidia biashara (ESOs) na kuziunganisha kupitia mtandao wa Tanzania Hubs Network. Sambamba na hilo, FUNGUO hutoa ushahidi, huleta wadau pamoja, na kusaidia majadiliano ya sera ili kushughulikia changamoto za kimfumo ambazo kwa kampuni au biashara changa hawawezi kupata suluhisho zenyewe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...