Na Janeth Raphael -MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Namibia kuchangamkia fursa zilizopo katika mataifa hayo mawili ili kuongeza kasi ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Juni 20, 2026, kufuatia mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, yaliyolenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili za Afrika.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia amesema Tanzania na Namibia zina historia ndefu ya ushirikiano iliyojengwa tangu harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa historia hiyo kugeuzwa kuwa faida ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia uchumi imara.
Amebainisha kuwa mwaka 2024, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Namibia ilikuwa takribani shilingi bilioni 20, akisema bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza zaidi kiwango hicho kupitia uwekezaji wa sekta mbalimbali.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijikita pia katika maeneo ya kimkakati ikiwemo usalama wa chakula, uchumi wa buluu, madini, mafuta na gesi, pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa pande zote mbili.
“Niwahamasishe wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa zilizopo Namibia, na pia wana-Namibia wafanye vivyo hivyo kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Rais Samia.
Katika sekta ya uchumi wa buluu, viongozi hao wamesema nchi zote mbili zina rasilimali kubwa za bahari zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, wakibainisha kuwa sekta hizo zina uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika.
Pia, mazungumzo yao yaligusia uwezekano wa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Namibia, hatua inayotarajiwa kurahisisha biashara, uwekezaji na kuongeza mtiririko wa utalii kati ya mataifa hayo mawili.
Rais Samia amesisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Afrika bado ni nguzo muhimu ya maendeleo, akieleza kuwa bara la Afrika lina rasilimali nyingi na nguvu kazi kubwa ya vijana ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa iwapo itatumika kikamilifu.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...