Na Janeth Raphael MichuziTv 

Serikali imewataka wanachama wa vyama vya ushirika nchini kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani ya Tanzania kwa kuchagua viongozi waadilifu, kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao na kusimamia rasilimali za ushirika kwa uwajibikaji ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo,  David Silinde (Mb), aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Julai 6, 2026, jijini Dodoma.

Akifunga maadhimisho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya "Ushirika kwa Dunia Yenye Amani," Mhe. Silinde alisema ushirika una nafasi kubwa katika kujenga mshikamano wa jamii na kudumisha utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya vyama vya ushirika hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu.

Amesema kila mwanaushirika ana wajibu wa kuwa mlinzi wa amani kwa kuhakikisha anashiriki katika uchaguzi wa viongozi waadilifu, kushiriki vikao vya vyama vyao na kutoa mchango katika maamuzi yanayolenga kuviimarisha vyama hivyo.

"Ushirika hustawi katika mazingira ya amani, mshikamano na ushirikiano. Hivyo, kila mwanaushirika ana jukumu la kulinda tunu hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa," alisema Mhe. Silinde.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alitoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na ubadhirifu wa mali za vyama vya ushirika, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia vibaya mali za wanachama au kukiuka sheria za usimamizi wa vyama vya ushirika.

Aidha, amewataka wanachama kuwa na utamaduni wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao, akieleza kuwa ushiriki wa wanachama ndiyo msingi wa kujenga vyama vyenye nguvu, uwajibikaji na uwezo wa kuchangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Msajili na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, alisema sekta ya ushirika inaendelea kupiga hatua kubwa kutokana na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Serikali, hususan matumizi ya mifumo ya kidijitali katika uendeshaji wa vyama vya ushirika.

Amesema matumizi ya teknolojia yameongeza uwazi, ufanisi, uadilifu na uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli za ushirika, sambamba na kuhakikisha sheria, kanuni na misingi ya utawala bora inazingatiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Federation of Cooperatives (TFC),  Tito Haule, alisema mchango wa sekta ya ushirika katika uchumi wa Taifa unaendelea kuongezeka kwa kasi, huku akibainisha kuwa mauzo ya mazao kupitia vyama vya ushirika yamefikia thamani ya shilingi trilioni nne.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha nafasi muhimu ya ushirika katika kuwawezesha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi, huku akitoa wito kwa wanachama kuendelea kuimarisha ushirikiano na kusimamia vyama vyao kwa uwajibikaji ili kuongeza tija na manufaa kwa wanachama pamoja na Taifa.

Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani mwaka 2026 yamehitimishwa kwa msisitizo wa kuendelea kuimarisha ushirika kama chombo muhimu cha kujenga uchumi shirikishi, kulinda amani na kuharakisha maendeleo endelevu nchini.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...