Airtel Money kwa kushirikiana na Buni,DTBI, Vocalize IoT Project na Techstar Innovation Hub* wamekutana na vijana kutoka vyuo vikuu na VETA nchi nzima kuwapa mafunzo ya Internet of Things - IoT na Digital Literacy.
Lengo ni moja tu: Kuwatengeneza vijana wawe wabunifu, waweze kujiajiri na kuzalisha ajira kupitia uchumi wa kidijitali. Hawataki tena vijana wawe watumiaji tu, wanataka wawe watengenezaji wa teknolojia zitakazotatua matatizo ya jamii.
Akizungumza na vijana hao, Meneja wa Huduma za Kifedha na Miamala ya Kigeni wa Airtel Money, Bi. Rita Nyamwehura alisema kampuni imeamua kuwekeza kwa vijana kwa sababu ndio chachu ya ukuaji wa uchumi.
"Airtel tumejikita kuhakikisha huduma zetu zinawafikia Watanzania popote walipo, mijini na vijijini, kwa njia salama, rahisi na yenye uhakika. Tunaamini teknolojia za kidijitali ni chachu ya ukuaji wa uchumi na fursa kwa vijana. Kupitia ushirikiano huu, tunataka kuwawezesha vijana kutumia ubunifu wao kutengeneza suluhisho zinazogusa maisha ya kila siku ya Watanzania," alisema Nyamwehura.
Pia aliwataka vijana watumie kikamilifu huduma za Airtel Money kama vile kununua vifurushi, kulipia bili, Lipa Namba na huduma nyingine ili waelewe jinsi teknolojia inavyoweza kuunganishwa na biashara.
Kwa upande wake, Bw. Elia Kinshaga kutoka JATEC ambaye ni Business Development Manager alisema mafunzo haya yanalenga kuwapa vijana uwezo wa kubuni teknolojia za IoT katika sekta za maji, usalama, usafirishaji, afya na utoaji wa huduma.
Alitoa mfano wa mita janja za maji zinazolipiwa kabla ya matumizi. Amesema teknolojia hizo zinapunguza upotevu wa mapato na kuongeza uwazi.
Kinshaga pia alifichua kuwa kupitia ushirikiano wa Airtel na DTBI kumekuwepo na Fursa Labs zenye vifaa vya kisasa vya TEHAMA - kompyuta, intaneti na maabara za ubunifu. Moja ya matunda yake ni mfumo wa Visomo unaomilikiwa na MagilaTech. Mfumo huu umesaidia wanafunzi wa VETA kusoma mtandaoni na sasa unatumika Tanzania, Dubai na DRC.
"Nawahimiza vijana kujiamini, kutumia maarifa wanayopata na kuendelea kubuni bidhaa na huduma za kidijitali zitakazochochea ajira na kuongeza tija," alisisitiza Kinshaga.
Mmoja wa washiriki, Levina Chifiye kutoka St. Joseph College of Engineering and Technology alisema mafunzo hayo yamefungua akili yake.
"Nimeelewa jinsi IoT inavyoweza kutumika kwenye usalama, usafirishaji na mifumo ya malipo. Pia Airtel Money API zitatuwezesha kuunganisha malipo kwenye miradi yetu ya kiteknolojia," alisema Levina.
Ushirikiano huu unaonyesha wazi kuwa mustakabali wa Tanzania upo mikononi mwa vijana wenye ubunifu na teknolojia.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...