Na Janeth Raphael - MichuziTv
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema juhudi zake za kuboresha mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi na ufugaji wa viumbe maji nchini zimeanza kuzaa matunda, baada ya kufanikiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa mazao ya uvuvi kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa, mafunzo kwa wachakataji na mifumo ya masoko ya kidijitali.
Muumin ameyabainisha hayo katika maonesho ya nanenane yanayoendelea jijini Dodoma ambapo amesema utekelezaji wa miradi hiyo, Afisa Mtaalamu wa Kitaifa wa Mnyororo wa Thamani wa Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji kutoka FAO, Hashim Muumin, amesema changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa ni upotevu wa samaki na mazao mengine ya uvuvi baada ya kuvuliwa kutokana na ukosefu wa miundombinu bora ya uhifadhi na uchakataji.
Ameeleza kuwa maeneo mengi yenye uzalishaji mkubwa wa samaki yako mbali na miundombinu muhimu, hali inayosababisha samaki kuharibika kabla ya kufikishwa sokoni. Aidha, alisema mifumo duni ya barafu, ukaushaji na uhifadhi ilikuwa ikichangia hasara kubwa kwa wavuvi na wachakataji.
"Mradi ulipoanza tulikuta kiwango cha upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa kikiwa takribani asilimia 40, na wakati wa msimu wa mvua kiwango hicho kiliongezeka zaidi kutokana na changamoto za ukaushaji na uhifadhi," amesema Muumin.
Kutokana na hali hiyo, FAO ilianzisha mafunzo kwa wachakataji wa samaki na dagaa kuhusu mbinu bora za uchakataji, ukaushaji na uhifadhi ili kuhakikisha bidhaa hizo zinafika sokoni zikiwa katika ubora unaokubalika na salama kwa matumizi.
Muumin amesema pamoja na mafunzo hayo, FAO imeweka mifumo ya kutengeneza barafu inayotumia nishati ya jua pamoja na mitambo mingine inayotumia umeme, hatua iliyosaidia kuongeza uwezo wa kuhifadhi samaki na kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao hayo.
Amesema uzalishaji wa barafu umeanza kuleta matokeo chanya, huku wavuvi na wachakataji wakinufaika kwa kupata muda mrefu wa kuhifadhi samaki kabla ya kuwafikisha sokoni.
Aidha, FAO ilifanya utafiti wa masoko uliobaini kuwa mahitaji makubwa ya samaki kutoka Ziwa Tanganyika yanapatikana katika mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Mwanza.
Kwa mujibu wa Muumin, utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 96 ya walaji wa samaki katika maeneo hayo wanapendelea samaki waliogandishwa (frozen), jambo lililoifanya FAO kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa barafu na kuwapatia baadhi ya wachakataji majokofu yanayotumia nishati ya jua, hasa katika maeneo ambayo huduma ya umeme bado ni changamoto.
Mbali na kuboresha uhifadhi wa samaki, FAO pia imeanzisha mfumo wa kidijitali unaojulikana kama Tan Fish Market (Tanzania Samaki) unaowaunganisha moja kwa moja wauzaji na wanunuzi wa samaki kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Kupitia mfumo huo, muuzaji huweka taarifa za samaki alionao, huku mnunuzi akifanya manunuzi kwa njia ya mtandao. Mfumo huo pia unarahisisha usafirishaji na malipo, hivyo kuhakikisha samaki wanawafikia wanunuzi wakiwa katika ubora unaohitajika.
Muumin amesema mfumo huo ulianza kutumika kwa wadau wa Ziwa Tanganyika, lakini tayari wadau kutoka Ziwa Victoria wameonyesha nia ya kujiunga kutokana na manufaa yake katika kupanua masoko na kuongeza kipato cha wavuvi.
Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa mradi huo kutoka mkoani Katavi, Amina Kasinge, ambaye ni mchakataji wa samaki na mmiliki wa vyombo vya uvuvi, amesema mafunzo na teknolojia walizopata kupitia FAO zimebadilisha shughuli zao kwa kiasi kikubwa.
Amesema kabla ya mradi huo walikumbwa na changamoto kubwa ya kuanika dagaa kwa ubora unaotakiwa, jambo lililosababisha hasara nyingi. Hata hivyo, baada ya kupata mafunzo ya uchakataji na mbinu bora za uhifadhi, wameongeza ubora wa bidhaa zao, kupunguza upotevu na kupata masoko yenye tija zaidi.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...